Thursday, 1 August 2013

Mwakyembe avutia pumzi `unga` airport

Kufuatia matukio mfululizo ya kukamatwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaodaiwa kuwa ni Watanzania kwenye viwanja vya ndege nje ya nchi wakipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema atalishughulikia suala hilo kama alivyofanya bandarini.

Dk. Mwakyembe ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo maalumu na NIPASHE kuhusu ufuatiliaji wa vitendo hivyo vinavyoharibu taswira ya nchi kimataifa.

Alisema anafahamu kila kitu kuhusu matukio ya dawa za kulevya, lakini anasubiri mamlaka zilizo chini yake kama vile TAA na bodi yake, uongozi wa JNIA na Polisi, ili wafurukute kwanza kama alivyofanya bandarini kwa lengo la kupima utendaji wao wa kazi.

“Mamlaka ni ‘system’, ina ngazi zake, kuna Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na bodi yake, kuna polisi, kuna uongozi wa uwanja wa ndege. Nataka muwabane kwanza hao ili wawaeleze hayo (ma)dawa ya kulevya yanapitaje hapo? Mimi najua kila kitu kuhusu kinachoendelea na iwapo wanawazungusha njooni kwangu,” alisema Mwakyembe na kuongeza:


“Haiwezekani ukaenda moja kwa moja kwa Rais, iwapo kuna suala linalomhusu Waziri, atakushangaa na kukuona huelewi kitu. Najua hatua ilipofikia na iwapo kuna mamlaka haijachukua hatua yoyote, mimi nitaishughulikia. Na kama imepita kote na imefikia kwa DPP, najua imefika ngazi ya kiwizara, ni lazima tulishughulikie.”

Dk. Mwakyembe aliongeza kuwa, anajua mtandao wa dawa za kulevya ni mrefu, lakini atashughulikia kama alivyofanya katika Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kwani baada ya kusikia ubovu unaotendeka aliwaacha wafurukute kwanza kwa takribani wiki mbili.

Alisema baada ya wiki hizo mbili akiwa na taarifa kamili kuhusu kilichokuwa kinaendelea, aliingia bandarini hapo na kuwafumua baadhi ya watendaji na kwamba ndivyo itakavyokuwa katika mamlaka zinazohusika na viwanja vya ndege kwani kwa sasa anasuburi kuona wanafanya nini kabla hajaingilia kati.

Agosti 27, mwaka jana, Waziri Mwakyembe aliunda Kamati ndogo ya Uchunguzi ya watu saba kubaini chanzo cha matatizo yanayozorotesha ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kukimbiwa na wateja wa ndani na nje ya nchi.

Baada ya uchunguzi huo, Dk. Mwakyembe aliwaondoa wajumbe wote wa Bodi ya TPA na kuteua wapya ili kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa taarifa hiyo. 

Juzi gazeti hili liliwasili katika ofisi za TAA, kwa lengo la kujua kinachoendelea kuhusu matukio hayo, lakini mmoja wa wafanyakazi katika ofisi hizo alisema Mkurugenzi wa mamlaka hiyo yupo, lakini asingeweza kuzungumza na waandishi bila kuruhusiwa kwanza na katibu wake wa mambo ya sheria, Ofisa Uhusiano na mwingine wa tatu ambao nao hawakuwapo hapo ofisini.

Mfanyakazi huyo wa kike ambaye alikataa kutaja jina lake wala cheo chake, alisema ofisi ya Mkurugezni ina watu watatu na utaratibu uliowekwa ofisini hapo ni kwamba, iwapo wafanyakazi hao wote hawapo, hakuna huduma itakayotolewa kwa mtu mwenye shida na Mkurugenzi kwa kuwa hataruhusiwa kumwona.

Hata hivyo, NIPASHE ilifanikiwa kumwona Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki, ambaye naye alidai kwamba, hawezi kuzungumzia sakata hilo kwa madai kwamba hashughulikii masuala ya dawa za kulevya.

Malaki alisema wanaohusika na suala hilo ni polisi kwa kuwa JNIA wanahusika na masuala ya wasafiri na kwamba anayeweza kuzungumzia sakata hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Suleiman Suleiman.

Wakati wa mazungumzo na gazeti hili ofisini kwake siku hiyo, Malaki, alimpigia simu Suleiman ambaye aliahidi kukutana na NIPASHE jana saa 5 asubuhi ili kutoa ufafanuzi wa sakata hilo.

Hata hivyo, jana mwandishi wa habari hizi alikwenda ofisini kwa Mkurugenzi huyo na kutaarifiwa kwamba amsubiri kidogo kwa sababu yupo kwenye kikao.

Hata hivyo, baada ya kusubiri kwa saa nne, katibu muhtasi wa mkurugenzi huyo alimweleza mwandishi kwamba bosi wake amekataa kuzungumzia jambo hadi atakapokuwa tayari.
"Mkurugenzi amesema hawezi kuzungumza tena na wewe hadi atakapopata muda wa kuongea na waandishi wa habari," alisema katibu ambaye hakutaja jina lake.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini, Deusdedit Kato, alisema kuwa, tayari wameshaandaa jalada la matukio hayo na juzi walilipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Hata hivyo jana, NIPASHE ilifika ofisini kwa DPP na kupewa taarifa ya kwamba yupo Dodoma kwa shughuli za kikazi hivyo msaidizi wake hawezi kuzungumzia lolote hadi yeye atakaporudi.
Julai 5, mwaka huu wasichana wawili wa Kitanzania walikamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine kilo 150 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8,  zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Tanzania.

Wasichana hao ambao ni Agness Gerald (25) na Melisa Edward (24), walikamatwa nchini humo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.

Ijumaa wiki iliyopita, taarifa kutoka Hong Kong, zilieleza kwamba maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Hong Kong (HKIA), walimkamata kijana mwenye umri wa miaka 25 akitokea Tanzania akiwa na dawa na za kulevya aina ya heroine kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bil.1.5 kwenye mzigo wake wa mkononi.

Taarifa zinaeleza zaidi kwamba, maofsa hao jioni siku hiyo hiyo walimkamata Mtanzania mwingene mwenye umri wa miaka 45 ambaye alipelekwa hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa aina ya heroine.

Mbali na hilo, pia Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.

Matukio hayo yametokea ikiwa ni takribani wiki moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Juni 28, mwaka huu kutangaza kuwa tatizo la dawa za kulenya hivi sasa ni janga la kitaifa.

Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.

Pia alisema katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, na hivyo kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment