Thursday, 1 August 2013

Unabii wa Nyerere unatimia kila uchao

Leo nitajadili unabii (nukuu za maneno) aliyosema Nyerere wakati wa uhai wake ili wasomaji wafanye tafakuri kama umetimia au la. Baada ya hapo tufanye utafiti kujua tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Je, tupo kwenye njia sahihi au tunafuata mkumbo wa ‘bora tufike?’

Akihutubia Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM mwaka 1987, Mwalimu Nyerere alisema: “Hatima ya nchi yetu ni jukumu letu sote. Kwa pamoja twaweza kuisaidia nchi yetu kusonga mbele kuelekea kwenye haki zaidi na usawa zaidi kwa Watanzania wote.”

Tujiulize: Tanzania ya leo kuna haki na usawa kwa wananchi wake? Inakuwaje leo, Jeshi la Polisi ambalo ni maalumu kwa usalama wa raia sasa limekuwa ‘uhasama dhidi ya raia?’ Raia hubambikiwa kesi, kunyimwa haki ya kuandamana, hupigwa na kuuawa. Baadhi ya hospitali zinakataa kupokea maiti zinazotoka kwenye mahabusu za polisi! 

Kumbuka hospitali ya Mwananyamala ilipokataa kupokea maiti aliyepelekwa na askari kutoka kituo cha Oyster Bay jijini Dar es Salaam wakati tayari kulikuwa na maiti mwingine aliyetokea kituo hicho hicho. N-nje ya hospitali hiyo ndugu wa marehemu walitaka kujua kutoka kwa polisi jinsi ndugu yao aliyechukuliwa nyumbani akiwa mzima na kupelekwa kusikojulikana na baadaye wakapewa habari kuwa kafariki!


Sasa tunasonga mbele, tumesimama au tunarudi nyuma? Elimu ni kama aliyotuachia Mwalimu Nyerere? Shule nyingi sasa hazina madawati na zingine zikiwa chini ya miti lakini watoto wa viongozi wanasomeshwa katika shule za taasisi za dini na watu binafsi. 

Baadhi ya mabenki na mashirika yakichangia ununuzi wa madawati, viongozi wetu bila aibu husimama kupongeza! Fedha za serikali zinazotumiwa ovyo kwa nini zisitumike kumaliza tatizo la madawati na kuwalipa walimu mishahara mizuri? 

Mwalimu alisema: “Lakini hata kama wageni wanaomiliki ardhi wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika  muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wenye ardhi na walio wengi wakiwa watwana.”

Haya ndiyo yanayotokea sasa katika mikoa mbalimbali nchini. Wananchi wanaporwa ardhi yao kwa kisingizio cha kupewa wawekezaji kumbe wawekezaji ni pamoja na viongozi wetu. Matokeo yake kumekuwa na migogoro ya ardhi kila siku kati ya wananchi na ‘wawekezaji.’ 

Hata mbuga za wanyama sasa viongozi wanashirikiana na ‘wawekezaji’ kugawana vitalu na kutorosha wanyama hai n-nje ya nchi!

Akiweka jiwe la msingi la shule ya sekondari ya wakimbizi kule Tunduru mwaka 1978, Mwalimu Nyerere alisema: “Watu wote waliumbwa sawa. Haiwezekani kikundi fulani cha watu kuendelea kuwakandamiza wengine. Aliyetuumba sawa atawapa nguvu wanaokandamizwa ili waweze kuwashinda wale walioamua kuwakandamiza wengine.” Migomo na maandamano yanayofanywa siku hizi ni ilani tosha kwa CCM kuwa kimechokwa.

Kuna usawa katika Tanzania ya leo? Viongozi wetu wanashindana kujilimbikizia utajiri kwa hali yoyote iwayo. Miiko ya uongozi haifuatwi wala wahusika hawajazi fomu kuainisha mali walizo nazo. 

Wakubwa wanaochota mabilioni ya fedha za umma wanafutiwa kesi kijanja kwa kunukuu vifungu hafifu vya sheria!  Ndiyo maana sasa wananchi wameichoka serikali ya CCM baada ya kupoteza dira ya maendeleo aliyotuachia Mwalimu Nyerere. 

Fedha za kuwapeleka wakubwa India na kwingineko kupata matibabu na  walizotengewa viongozi wastaafu kwa ajili ya matibabu kila mwaka zingeweza kabisa kununua vifaa-tiba vya kisasa katika hospitali zetu za rufaa. 

Badala yake tumekuwa wepesi wa kupeleka wagonjwa Nairobi, Afrika Kusini, India, Uingereza, Ujerumani n.k. kutokana na hospitali zetu kukosa si vifaa-tiba mujarabu tu, bali hata dawa stahiki.

Kina ‘pangu-pakavu’ hufia humu humu nchini kwa ukosefu wa fedha za kujitibu. Hujaona matangazo yanayotoka kwenye vituo vyetu vya runinga watu mbalimbali (wakiwamo watoto) wakiomba msaada wa fedha za kuwapeleka kwenye tiba n-je ya nchi? Majuzi tu tuliona wagonjwa wa figo waliolazwa kwenye hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam wakiomba msaada wa serikali kuwapeleka India kupata matibabu. 

Kama serikali inashindwa kuwahudumia raia wake, usawa unaosemwa majukwaani u’ wapi?
Katika kitabu cha Azimio la Arusha, Mwalimu aliandika: “Ni ujinga kutegemea pesa kama chombo cha maendeleo wakati tunafahamu vyema kwamba nchi yetu ni masikini. 

Lakini ni ujinga zaidi kufikiria kwamba tutajikomboa kutoka kwenye umasikini wetu kwa kutegemea misaada ya kigeni badala ya juhudi zetu wenyewe.”

Juhudi zetu wenyewe ni mashamba, majumba na viwanda vilivyotokana na Azimio la Arusha na kuwapatia ajira maelfu ya raia. 

Vyote hivyo vimebinafsishwa kijanja huku viongozi wakiwa miongoni mwa wamiliki na ajira ya maelfu kufutwa. Migodi iliyoenea kila eneo la Tanzania, imekuwa ikiwanufaisha wageni huku wananchi wakifukuzwa kutoka maeneo yao na serikali kuambulia mrabaha wa asilimia tatu na ‘wawekezaji’ kuhamisha asilimia 97 kwa kisingizo kuwa hawajapata faida!

Akihutubia Bunge mwaka 1966, Mwalimu  Nyerere alisema: “Taifa letu limejijengea heshima ya kutopoteza fedha za umma kwa mambo yasiyo na umuhimu mkubwa. Hata hivyo lazima tuendelee kupunguza ukubwa wa misafara yetu n-nje ya nchi. Aidha tusikubali tu mialiko ya n-nje kwa kuwa tunalipiwa nauli na kila kitu. Hali hiyo itatufanya tusiwe huru wakati wa majadiliano.”

Mawaziri wa Kikwete wanavurunda katika mambo mengi lakini waamekuwa hawachukukuliwi hatua zozote.
Ndiyo maana Mwalimu Nyerere alisema: “Mawaziri wanapofanya makosa makubwa na badala ya kujiuzulu wanaanza kufanya hila na kutafuta visingizio vya kutofanya hivyo, ni wajibu wa Rais kuwafukuza, maana hiyo ni kazi yake mwenyewe asiyoweza kusaidiwa na mtu mwingine.”

Wakati huu ambapo kuna urani kule Ruvuma, Dodoma na Kilimanjaro, dhahabu karibu kila mkoa wa Tanzania, almasi, tanzanite, shaba, chuma, makaa ya mawe, mafuta, gesi asilia n.k. tutapata ‘wawekezaji’ watakaotulaghai kwa misaada ya hapa na pale nao watajichotea utajiri wetu na kutuacha na umasikini wa kujitakia! Mwalimu alipata kusema “uchumi tunao lakini tunaukalia.” Wahenga walikuwa sahihi kusema “penye miti hapana wajenzi.”

Nyerere alisema: “… umasikini m-baya kuliko wote ni umasikini wa mawazo. Duniani kuna kujitegemea na kutegemea. Unaweza kutegemea,  lakini kutegemea kokote ni kubaya sana. Kwa hali yoyote ile, kutegemea kubaya kupita kote ni kumtegemea mtu mwingine kwa mawazo. Ni kwa ovyo sana na kunakunyima utu wako.”

Matokeo ya kuzitegemea sana nchi za n-nje ndio haya tuyaonayo sasa. Zaidi ya nusu ya bajeti zetu hutegemea hisani na ufadhili wa nchi za n-nje. Tunaelekezwa na kupangiwa namna ya kupanga mipango yetu ya maendeleo na utekelezaji wake na vitisho vya kutosaidiwa iwapo tutakiuka makubaliano. Ndiyo umasikini wa mawazo aliosema Nyerere.

Hivi sasa wakati nchi inajiandaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015, tayari kuna hekaheka zinazofanywa na wanaotafuta kwa udi na uvumba kupendekezwa kugombea kiti cha urais. Hekaheka hizo ni pamoja na kasi ya kugawa fedha kama peremende kwenye nyumba za ibada kwa kile kinachoitwa ‘harambee’ za ujenzi wa makanisa na misikiti.

Akiwaelekeza Watanzania kumchagua rais bora badala ya bora rais, Nyerere alipata kusema: “Kulazimika kumchukulia hatua rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote ile. Ndiyo maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu mkubwa na wakisha chaguliwa wanatakiwa wajiheshimu na kuwa waangalifu sana.”

Kwa nini kasi hii ya kugawa mamilioni kwenye nyumba za ibada inafanywa sasa? Hao wanaotoa na kukanusha kuwa wao ni matajiri, wanazitoa wapi fedha hizo? Majimbo wanamotoka yamesitawi kiasi cha kutokuwa na haja ya kuendelezwa zaidi? Kama bado, kwa nini wanawaacha wapiga kura wao katika umasikini na dhiki nao wanamwaga fedha kila uchao kwenye nyumba za ibada? 

Marafiki wanaowasaidia kuchangia katika harambee hizo hutoa wapi fedha kila mara na malengo yao ni nini iwapo mwenzao atafanikiwa kuwa rais wa nchi?

Lazima wananchi wawe makini na watu wanaojipitisha kwao na kwenye  nyumba za ibada kujifanya wasamaria na wachangiaji wazuri kumbe wana ajenda iliyojificha. Anayepita kugawa hela na kuwanunua wananchi kwa lengo la kutaka achaguliwe kwenye nafasi ya uongozi, hafa

No comments:

Post a Comment