Ofisi ya walimu pamoja na vyumba vinne vya madarasa ya shule ya msingi Mzee Chalinze wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, viko hatarini kubomoka kutokana na uchakavu uliokithiri hali iliyosababisha Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuhamishia ofisi yake katika choo cha wavulana.
Shule hiyo yenye wanafunzi 450 wa darasa la kwanza hadi la saba wanalazimika kusoma kwa awamu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, kwani kwa sasa kuna vyumba vitatu tu vinavyotumika kati ya nane vinavyohitajika.
Aidha, vyumba vitano vya madarasa shuleni hapo vilifungwa na kamati ya shule pamoja na wazazi kutokana na kuwa na miundombinu chakavu.
Mwalim Mkuu wa shule hiyo, Elias Kapama, alisema jana kuwa hatua ya kuihama ofisi yake imefika baada ya kutawaliwa na hofu na kutofanya kazi zake kama inavyotakiwa baada ya ofisi aliyokuwa akitumia kupasuka nyufa nyingi na kutishia kuanguka wakati wowote.
Aliitupia lawama Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kushindwa kuchukuwa hatua licha kuona amehamishia ofisi yake katika jengo la vyoo vya wanafunzi ambavyo havijaanza kutumika tangu ujenzi wake ukamilike mwaka 2011.
"Najisikia vibaya hata kwa wanafunzi wanapoona natumia chumba maalumu cha kubadilishia nguo cha wavulana katika choo chao ambacho walipaswa watumie wao, lakini sina jinsi ya kuepuka hili ni vema serikali ikafanya jitihada za makusudi katika kuhakikisha ofisi yangu, vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu zinajengwa kwa haraka," alisema Kapama.
Hata hivyo, mwalimu mkuu huyo alisema vyoo hivyo ambavyo anatumia kama ofisi vilijengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Ebenezer Spiritual Center ya mjini Chalinze vimegharimu kiasi cha Sh. milioni 70 hadi kukamilika.
Mwalimu mkuu huyo aliongeza kuwa kwa sasa walimu wanatumia tundu moja la choo huku wanafunzi 450 wakitumia matundu saba, wasichana matundu matatu na wavulana matundu manne.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment