Thursday, 5 September 2013

Mnigeria adakwa na ‘unga’ JNIA

RAI wa Nigeria, Ojo Athnonie (25) amekamatwa na dawa zinazosadikiwa kuwa za kulevya, pipi 99 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza jana na Tanzania Daima, Meneja Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, alisema kuwa binti huyo aliingia nchini Agosti 30, mwaka huo akitokea nchini Nigeria.
Alisema kuwa binti huyo alikamatwa katika uwanja huo wakati akiwa katika harakati za kuondoka na ndege ya Shirika la Ethiopia saa 8:00 mchana kuelekea nchini Ufaransa.
Jingu alisema kuwa pipi hizo zilibainika kuhifadhiwa ndani ya chupa za poda (Johnson) baada ya kufanyiwa upekuzi wa kina wa mizigo aliyokuwa ameibeba.
“Ni kweli tukio hilo limetokea jana wakati binti huyo akiwa katika harakati za kuondoka kuelekea nchini Ufaransa na kisha Nigeria, hivyo maofisa walilitilia shaka begi lake na ikawalazimu kulifanyia ukaguzi zaidi kwenye eneo la mashine ya X-ray ndipo zilipobainika pipi hizo,” alisema.
Meneja huyo alisema kuwa baada ya tukio hilo, polisi waliizuia safari yake na kuchukua pipi hizo kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi ili kuweza kubaina aina ya dawa hizo.

No comments:

Post a Comment