VILIO na watu kuzirai ni matukio yaliyotawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa waKilimanjaro wakati wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa bilionea wa madini jijini Arusha, Erasto Msuya (43) inayowakabili washtakiwa watatu.
Msuya alipigwa risasi zaidi ya 10 kifuani mwezi uliopita karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Kilimanjaro (KAI) na kupoteza maisha papo hapo.
Matukio hayo ya vilio na watu kuzirai yalianza mahakamani hapo jana saa 5:7 asubuhi na kudumu kwa takriban dakika 10 baada ya kesi hiyo kuahirishwa tena hadi Septemba 18 mwaka huu, kutokana na upelelezi kutokamilika, hivyo washtakiwa hao kurejeshwa rumande kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana.
Walioangua vilio na kupoteza fahamu ni dada wa marehemu, Antuja Msuya na mdogo wake Bahati Msuya, ambao ni wakazi wa Arusha na Mererani, hivyo kusababisha usumbufu kwa muda mahakamni hapo.
Mapema kabla ya tukio hilo, Wakili wa Serikali, Stella Majaliwa, aliieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Theotmus Swai, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Alisema kuwa mshitakiwa wa pili, Shaibu Jumanne, maarufu kama Mredi (38), hakuweza kufika mahakamani hapo kutokana na kuugua.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hii ilikuwa inakuja mahakamani hapa kwa ajili ya kutajwa, tunaomba tarehe nyingine. Mtuhumiwa wa pili hakuweza kufika kwa sababu anaugua,” alisema.
Wakili Hudson Ndusyepo anayewatetea mshitakiwa wa kwanza na watatu aliiomba mahakama hiyo kuuagiza upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wa shauri hilo haraka ili kuwatendea haki wateja wake.
Juzi, Jeshi la Polisi mkoani hapa lilitangaza kumtia mbaroni mtuhumiwa mwingine ambaye pia ni mfanyabiashara wa madini akidaiwa kuhusika kupanga njama za mauaji ya Msuya.
Aliyekamatwa ni Joseph Damas, maarufu kama Chusa (36), ambaye alinaswa mkoani Arusha na kisha kuletwa Kilimanjaro kwa ajili ya mahojiano na polisi.
Taarifa zilizopatikana jana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, zilieleza kuwa huenda mtuhumiwa huyo jana angeongezwa katika kesi hiyo ya mauaji inayowakabili watuhumiwa wengine, Sharif Athuman (31) mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha pamoja na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu, Arusha.
“Leo kwenye kesi ya mauaji ya Msuya ataongezwa mtuhumiwa Joseph Damas aliyeshiriki na kupanga mauaji hayo,” ilieleza taarifa hiyo ya Kamanda Boaz kwa waandishi wa habari.
Alipoulizwa sababu za mtuhumiwa huyo kutoonekana mahakamani kama alivyodai katika taarifa yake ya mapema, Kamanda Boaz alisema kuwa upelelezi haujakamilika na kwamba alikuwa wilayani Same akihudhuria kikao cha maofisa.
Kesi hiyo ya mauaji namba 06 ya mwaka 2013, iliahirishwa hadi Septemba 18, mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Washitakiwa hao, wanakabiliwa na kosa la mauaji ya kukusudia, kinyume cha kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 ya mwaka 2012.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment