Wednesday, 4 September 2013
Mtoto wa miaka 7 kulea wadogo zake mwenye msaada wasiliana 0713612533
SIKU chache baada ya gazeti dada na hili la Amani kuandika habari ya mtoto wa miaka 7, Sara Shija kuilea familia bila msaada wa wazazi wake, mambo mazito zaidi yamefichuka.
Mara baada ya taarifa za habari hiyo kutapakaa mitaani, imebainika kwamba baba mzazi wa familia hiyo inayoishi Bangulo, Kata ya Pugu amefungwa.
Risasi Mchanganyiko limeongea na mjumbe wa eneo wanaloishi watoto hao, Juma Kabuwa ambaye alithibitisha kufungwa kwa mzazi wa watoto hao aitwaye Shija.
“Baba yao alipoondoka nyumbani alikwenda Kibaha Maili Moja, huko kwa rafiki yake akakutana na mgogoro wa kugombea shamba ndipo alipofungwa jela,” alisema mjumbe huyo.
Akifafanua zaidi, mjumbe huyo alisema bwana Shija alienda Kibaha kwa rafiki yake ambaye ndiye aliyekuwa kwenye mgogoro huo wa shamba na yeye akaingia kumsaidia ndipo alipokamatwa na polisi na kuwekwa ndani.
Mjumbe huyo alisema kuwa taarifa hizo alizipata baada ya kutoka kwa gazeti hili na yeye kuanza kufuatilia kisa cha bwana Shija kuikacha familia yake.
“Awali nilikuwa sijui kitu chochote ila baada ya kutoka kwa gazeti lenu ndipo nilipoambiwa kuwa Shija amekamatwa na hakukuwa na mtu wa kumwekea dhamana,” alisema.
Mjumbe huyo alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha Shija kushindwa kumpa taarifa kwani wamekuwa wakishirikiana katika mambo mengi kiasi kwamba angeweza kuangalia hatima ya watoto wake.
Hata hivyo, mpaka dakika hii, hakuna anayejua alipo mama mzazi wa watoto hao ambao wanaishi katika mazingira magumu baada ya wazazi wao kuwaacha na kumfanya Sarah kuwalea wenzake watatu.
Katika hali hiyo, watoto hao wamekuwa wakinywa maji machafu na kushindwa kupata mahitaji muhimu ya chakula huku wakiwa hawana uangalizi.
Kama kuna ndugu anayewafahamu watoto hao au mtu anayetaka kuwasaidia awasaliane na chumba cha habari kwa simu 0713612533.
chanzo:globalpublishers
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment