Thursday, 19 September 2013

Mwalimu anaswa na majibu darasa la saba

JESHI  la  polisi  mkoani hapa, linamshikilia mwalimu wa  shule ya msingi Makungu, wilaya ya  Mufindi, Edwin Ambukile kwa tuhuma  za  kuwasaidia majibu wanafunzi wa  darasa la  saba katika mtihani  wa taifa uliomalizika hivi karibuni. 
Kamanda  wa polisi mkoa  wa Iringa, Ramadhan Mungi, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa  tukio  hilo lilitokea  Septemba 15 mwaka  huu.
Alisema mwalimu  huyo ambaye anafundisha masomo ya sayansi pia alikuwa mwalimu wa masomo ya ziada katika  shule  hiyo.
Alisema kuwa  sababu ya  kuwasaidia  wanafunzi majibu ni kutaka  kupata umaarufu kwa wanafunzi  watano aliokuwa akiwafundisha masomo ya  ziada ambapo aliapa kwamba lazima watafaulu kwa alama za juu.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, Septemba 11  alipokea mitihani kutoka kwa msimamizi  na baada ya hapo akafungua bahasha   ya masomo ya  sayansi na kuanza  kufanya mwenyewe  na majibu kuyatuma kwa njia ya ujumbe mfupi kwa  mke  wake.
“Siku ya mtihani, mmoja kati ya wanafunzi  waliopata majibu hayo alipoingia katika  chumba  cha mtihani, alionekana akitetemeka  kupita  kiasi, hivyo msimamizi wa mitihani alipompekua, alimkuta na majibu hayo na kueleza jinsi alivyosaidiwa na mwalimu  huyo,” alisema Kamanda Mungi.
Alisema mwalimu Ambukile  anatarajiwa kufikishwa mahakamani  wakati  wowote kuanzia sasa.
Chanzo:daima

No comments:

Post a Comment