Monday, 25 November 2013

Profesa Juma Kapuya, kudaiwa kutoweka nchini kukwepa mkono wa sheria.

SIKU chache baada ya Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), kudaiwa kutoweka nchini kukwepa mkono wa sheria dhidi ya tuhuma za kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka, vigogo wa polisi wanadaiwa kuhusika kumsaidia kutimkia nje, Tanzania Daima limedokezwa.
Habari ambazo gazeti hili limezipata, zinaeleza kuwa siku mbunge huyo akikamilisha taratibu za kusafiri, ndiyo siku ambayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni lilikuwa limekamilisha kufungua jalada la tuhuma zake na liliweka mtego wa kumnasa.
“Wakati Polisi Kinondoni wakiweka mtego wa kumnasa, baadhi ya polisi walimjulisha na hata kumsaidia kuhakikisha anasafiri nje ya nchi,” alisema mmoja wa maofisa wa juu wa polisi nchini.
Hata hivyo, kuna utata na kauli zinazopingana kuhusu mbunge huyo. Taarifa nyingine zinasema kuwa mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri, anadaiwa kusafiri kwenda nchini Sweden kwa masuala ya kikazi, na kwamba atakuwepo huko kwa muda usiopungua mwezi mmoja.
Chanzo kingine kimedokeza kuwa mbunge huyo alidai ametumwa kazi na kigogo mmoja serikalini na atakuwepo nchini humo miezi miwili hadi mitatu.
Hata hivyo, haijajulikana kazi anayokwenda kuifanya Kapuya ingawa kuna taarifa safari hiyo imelenga kutuliza upepo mbaya wa kuandamwa na tuhuma za ubakaji ambazo zipo polisi hivi sasa.
Tayari Profesa Kapuya alishafunguliwa jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam juzi.
Hata hivyo Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linamsaka mbunge huyo ndani na nje ya nchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikaririwa juzi kuwa watamtafuta Kapuya nchi yoyote atakayokwenda iwapo tuhuma dhidi yake zitathibitika.
Alisema mtandao wa polisi ni mkubwa, hivyo si rahisi kwa mtuhumiwa yeyote kuukwepa mkono wa sheria endapo itahitajika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Sisi tunashirikiana na polisi wa nchi mbalimbali duniani, ndiyo maana inakuwa rahisi kwa mtuhumiwa aliyetoroka nchi fulani kukamatwa nyingine na kurejeshwa kwao.
“Nataka niwaondoe hofu wale wote wanaodhani polisi haiwezi kumkamata mtu akikimbia nchini, tuna mkono mrefu sana, na hatufanyi kazi kinyume na taratibu zetu,” alisema.
Kamanda Wambura pia alikiri polisi kufungua jalada la Kapuya, huku akiweka wazi kuwa kinachofanyika hivi sasa ni uchunguzi wa tuhuma zake.
Alisema miongoni mwa maeneo wanayoyafanyia uchunguzi ni kubaini kama ujumbe ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha unatoka katika simu ya mbunge huyo.
“Tumefungua jalada, lipo kwa ajili ya uchunguzi na tukibaini kuwa ni nani anahusika na tuhuma hizo tutamsaka na kumkamata popote alipo,” alisema Wambura.
Gazeti hili limekuwa likiandika namba ya simu ya Prof. Kapuya ambayo huwa anaitumia kutuma ujumbe wa vitisho kwa binti huyo, ingawa kuna vyombo vingine vya habari viliamua kuandika kwa mtazamo tofauti na kumtuhumu dada wa binti aliyebakwa kuwa ni mtu mzima na kuwa ana uhusiano na Kapuya, na wana watoto.
Simu hiyo namba 0784993930 inayodaiwa kumilikiwa na Profesa Kapuya, mbali ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno ya kutishia kuua, pia ndiyo inayodaiwa kutumika kutuma pesa kwa njia ya mtandao kwenda kwa binti huyo.
Tangu gazeti hili lianze kuandika tuhuma hizi nzito, kumekuwapo na kusuasua kwa mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani na Jeshi la Polisi.
Harakati za kufungua jalada dhidi ya Kapuya zilizoanza wiki iliyopita ziliendelea hadi juzi ambapo polisi walitumia zaidi ya saa 12 kumhoji binti huyo anayedaiwa kubakwa ili kupata ukweli wa sakata hilo.
Akiwa polisi, binti huyo alikutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na kutoa maelezo ya awali kabla ya viongozi hao kumruhusu ayaweke malalamiko yake katika maandishi kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment