Monday, 30 December 2013

Kwanini wanandoa huwa na mapenzi ya dhati mwanzoni tu, kisha huchuja?

 

Kumbe mambo yalianza kwa furaha, ibilisi akaingilia kati, mikataba ya ndoa mbele za viongozi wetu wa dini ikavunjwa na matokeo yake waliopeana nyama za ulimi (maneno matamu) sasa wanapigana visogo. Kulikoni?  Sikia ujumbe huu halafu nawe useme.
 
 
Utawakuta wanandoa wengine wanatumia gari moja ya familia kwenda kazini wanaweza kutoka nyumbani mpaka makazini mwao hutaona kicheko wala tabasamu, wamenuna hao utashangaa!
 
Utakuta wengine wakitoka nyumbani furaha tele wanatamani wasifike upesi. Utawaona kwenye foleni wakicheka, wakikumbatiana utajua tu hawa ni wapenzi wapya. 
 
Wapo wale wenzangu na mimi utakuta ametoka nyumbani kanuna na akifika kazini vicheko vingiii… lakini akirudi nyumbani kanuna.  
 
 
Unajua pale mwanzoni bado yale mapenzi ya kabla ya uchumba, kisha ndoa yanakuwa bado moto moto. Kila kitu wanaelezana na ikiwezekana kila mahali kwenye mialiko au kutembelea ndugu wanaongozana au wanapeana ruksa.
 
Ngoja azaliwe mtoto wa kwanza. Kasi ya penzi inaanza kupungua hasa kutokana na ukweli kwamba mama anaanza kuweka mkazo zaidi katika kumlea mwanae, huku baba naye akipata fursa ya kuchati na marafiki zake na pia kujikita zaidi katika kazi.
 
Kadiri watoto wanavyoongezeka ndivyo penzi linapungua na wivu unachipuka. Mama yuko bize na watoto, baba naye anapata mwanya wa kufanya mambo yake na ndipo pia anapopata fursa ya kutafuta mahusiano ya nje au kurejea mchuchu wa awali kabla ya ndoa kama alikuwa naye.
 
Wengine ndipo huanza kuchelewa kurejea nyumbani na kumfanya mama aanze kuuliza kulikoni. Kwa kinababa wengine huanza kuwa wakali wanapoulizwa na kuanza kutoa kauli za kukatisha tamaa. 
 
Hawa wako wengi tu wenye mtindo huo. Ukiona hivyo ujue nyumbani huko moto unawaka hakukaliki. Lazima wameamka na visirani vya jana yake pengine mume alichelewa kurudi, mke alitoka bila kutoa taarifa au kuna kutoelewana katika jambo fulani la kifamilia na kadhalika.
 
Na watu wa aina hii wengine wana makubwa zaidi yaliyojificha. Kwa mfano, kama wanalala kitanda kimoja na visirani vyao, basi watalala mzungu wa nne si unajua (kama sikosei) ile karata ‘K’ ambayo wazungu wamegeuka kwa kichwa ni mguuni na mguuni ni kichwani. Upo hapo?
 
Au mke na mume wamegeuziana migongo huyu anatizama ukutani na mwingine anageukia mbele ya kitanda. Ukiona hivyo ndoa imeingia shubiri.
 
Wengine baba analala chumba cha ndoa, mama analala sebuleni au chumba cha watoto. Sekeseke za aina hii ziko tele majumbani mwetu lakini wahusika wanakaa kimya. Ndio hao ukiwaona ndani ya magari yao makubwa wamenuna kama nini. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.
 
Lingine alilouliza ni kwanini wanandoa wengine wakitoka nyumbani furaha tele wanatamani wasifike upesi. Ndani ya magari yao wanacheka hadi raha. Hawa wamejenga msingi mzuri wa ndoa yao na kila mmoja anamwelewa mwenzake.
 
Kila mmoja ameshayafahamu madhaifu ya mwenzake na ikitokea hitilafu wanajua namna ya kurekebisha na maisha yasonga mbele. 
 
Hivyo ndivyo inavyotakiwa. Maisha ni maelewano na kurekebishana kwani hakuna aliye kamili ila Muumba Mwenyezi Mungu pekee.
 
Lingine alilouliza ni kwanini wanandoa wakitoka nyumbani wamenuna lakini wakifika kazini vicheko vingiii… kisha wakirudi nyumbani wananuna tena. Hawa wanaficha machafu yao. Utakuta kule ofisini yupo mtu anamzuzua hivyo kwamba nyumbani hana habari.
 
Huyu kama ni mke hata haki ya ndoa kwa mumewe humnyima, kisa huko nje ana mchuchu wa kujidai, jambo ambalo siyo sahihi. Hawa ndiyo wanaoleta hata maradhi mabaya nyumbani. 
 
Tabia hii iko pande zote kwa mwanamke na mwanaume. Ikifikia hapo ndipo utaona wanaporejea nyumba zao za ndoa wananuna hawaonyeshi ucheshi wa awali, kisa wamepata vyungu vipya huko maofisini au mitaani. Upo hapo? Habari ndiyo hiyo bila hata chenga
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment