MSANII wa filamu za vichekesho, Ulimboka Mwakasala ‘Senga’, amesema kwa sasa anapumzika kucheza filamu hizo na kuhamia za kawaida.
Senga ni miongoni mwa wasanii wakongwe ambao wanatamba katika tasnia hiyo, kutokana na ubora wa kazi zao pamoja na uwezo mkubwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Senga alisema soko la filamu hizo haliuzi, zaidi ni kuuza sura zao bila wao kupata mafanikio.
“Sanaa ya vichekesho ipo kwa ajili ya kuuza sura tu na si kujipatia kipato sisi waigizaji, kuanzia leo nimetangaza rasmi kuachana na filamu za vichesho, nitacheza endapo mkataba utakuwa wa hela nzuri na si kama tulivyozoeshwa,” alisema.
Senga alisema anaamini filamu za kawaida zina faida kwake, kwani hivi karibuni kacheza filamu mpya ya ‘Madame’ ambayo ni ya Wema Sepetu na imemlipa sana na kumfanya asahau kabisa vichekesho.
“Nimecheza filamu ya Wema, imenilipa vizuri sana, nafikiri ningekuwepo kwa muda mrefu katika filamu hizi ningekuwa nimefanikiwa, lakini nilikokuwa nilikuwa nauza sura na sikuwa nanufaika na kitu,” alisema Senga.
chanzo: tz daima
No comments:
Post a Comment