Monday 31 March 2014

Walioachika, wasiooa kufa mapema??????????

Naam. Utafiti mpya wa masuala ya uhusiano umebainisha kuwa watu wenye umri kati ya miaka 35 na 40, ambao hawajaoa au kuolewa wapo kwenye hatari ya kufa mapema tofauti na waliooa au kuolewa.

Matokeo ya utafiti huo, uliofanywa kipindi cha karibuni na wataalamu wa masuala ya uhusiano , ukiongozwa Dk Ilene Siegler wa Idara ya Sayansi ya Tabia kutoka Chuo Kikuu kilichopo Kaskazini mwa  Jimbo la Carolinanchini Marekani, umebainisha pia kwamba ndoa ni kinga inayomwongezea binadamu muda wa kuishi.

Aidha, watafiti hao wamebainisha kwamba wanawake waliopewa talaka au kufiwa na wenza katika umri wa kati wapo kwenye hatari ya kufa mapema zaidi.


Watafiti hao wameeleza kuwa watu ambao maishani hawajawahi kuoa au kuolewa, wapo kwenye hatari ya kufa mapema mara tatu zaidi ya wale waliokuwa katika ndoa imara katika maisha yao, hasa wakiwa kwenye umri wa kati.

Matokeo hayo ambayo yalichapishwa kwenye jarida la  Annals journal  la Marekani na kuandikwa kwenye mtandao wa Daily Mail, ulihusisha watu 4,802, wakiwamo watu waliozaliwa miaka 40 iliyopita.

Ulibaini kuwa kati ya watu wazima wenye umri kama huo,  wengi wao walikufa wakiwa na miaka 50, kutokana na kuishi peke yao.

Kwa kutumia dodoso na maswali ya moja kwa moja, walibaini kuwa pamoja na mtu aliyekuwa kwenye ndoa kuishi kwenye maisha hatarishi kwa kunywa pombe kupita kiasi na kuvuta sigara, bado walio kwenye ndoa wana nafasi ya kuishi muda mrefu zaidi kwa asilimia 2.3.

Dk. Ilene Siegler, anasema kuwa maisha ya kwenye ndoa ni kinga inayowafanya wanandoa waishi kwa muda mrefu. “Inaonyesha kuwa na mke au mume ni kinga ya maisha hasa katika umri wa kati, hali hii ikiwaathiri zaidi wanaume, kuliko wanawake,”amesema Siegler.

Alisema kuwa utafiti huo umewawezesha kubaini kuwa kati ya vifo 238 vilivyotokana na athari za kutokuoa au kuolewa, wanaume ndiyo waliothirika zaidi na kwamba kati yao wanawake walikuwa ni 32 tu.

Alifafanua kuwa wanaume wameathirika zaidi kutokana na kutokuwa karibu na familia, hivyo kufanya mambo tofauti na mwanamke, ambao hata kama hajaolewa anaweza kuwa karibu na familia na kupata ushauri wa baadhi ya mambo, ingawa hali hiyo haimfanyi kuwa salama,”anasema Siegler.

Dk. Siegler alitolea mfano utafiti uliofanywa hivi karibuni na nchi saba za Ulaya akieleza kwamba utafiti huo umeonyesha kuwa mtu aliye kwenye ndoa huwa na furaha kimwili, kiakili  na kiafya na humfanya awe na marafiki wazuri, pia hupata ulinzi kwa kuwa wanandoa wana kawaida ya kujilinda wenyewe. 

Mtaalamu huyo aliendelea kuutoa ushahidi wa tafiti mbalimbali alizoziona akisema kuwa utafiti kutokaSweden unaonyesha kuwa wakati ndoa humlinda mhusika dhidi ya maradhi ya Alzheimers, wanaoishi na mpenzi wakiwa kwenye umri wa kati wapo kwenye hatari ya kupata matatizo ya akili.

“Kwa mujibu wa utafiti huo wa Sweden ni kwamba wanawake waliopewa talaka au kufiwa na mwenza kwenye umri wa kati wapo kwenye hatari ya kufa mapema mara tatu zaidi,”anabainisha Siegler.

Matokeo hayo ya utafiti yanaungwa mkono na Dk. Rebeka Sima wa Idara ya Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akieleza kuwa kwa kawaida, binadamu yeyote ni lazima awe kwenye uhusiano.

Anasema kwamba kama binadamu hayupo kwenye uhusiano ni lazima atakuwa na upungufu fulani, ambao kibinadamu ni maradhi, ikiwamo msongo wa mawazo na mengine yanayofanana na hayo.

“Hata iweje, wanandoa wanakuwa wanaaminiana kiasi cha kupeana ushauri. Sasa kwa kuwa mpweke ni lazima mhusika atakosa mtu wa kushauriana naye jambo linalosababisha kusononeka na pengine hata kuongea peke yake, kitu ambacho ni hatari zaidi,” anaeleza Dk Sima akiongeza:

“Mpenzi anaweza kuwa wa siku moja au mbili au hata zaidi, lakini uaminifu kati ya mke au mume ni kitu kingine, hivyo walio kwenye uhusiano wa namna hiyo huwa kwenye hatari zaidi kwa kuwa huongeza msongo wa mawazo kutokana na kutokuwa na uaminifu kati ya wahusika.”

Alifafanua kuwa kwa tamaduni za Kiafrika mtu ambaye hajaoa au kuolewa hawezi kutoa ushauri au kuchangia lolote kama walio kwenye ndoa, hivyo mhusika hujitenga mwenyewe kwa kuhisi anadharauliwa, jambo litakalomfanya awe mpweke na kufanya mambo ya kukurupuka.

Naye Modesta Kimonga ambaye ni mtaalamu wa masuala ya saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dodoma alisema kuwa binadamu akishakuwa mtu mzima anakuwa na uamuzi binafsi kwa mambo yake na kwamba  akiwa na mwenza, mara nyingi hukumbushwa yaliyo mema na kukatazwa mabaya hali ambayo kwa asilimia kubwa husaidia kumfanya mhusika aache mabaya kila anapokumbuka kuwa alikatazwa na mwenza wake.

“Hata kama wanagombana kwa kiasi gani ni lazima kuna baadhi ya mambo wanashuriana, hasa  kwenye matatizo ya kifamilia na kwenye masuala ya msingi kwa mfano matatizo kazini, ugonjwa na mambo kama hayo. 
chanzo:nipashe

Hivyo kuna muda ni lazima kwa mtu mzima kuwa na mwenza wake karibu hii humsaidia sana kupata faraja na kuongeza siku za kuishi,”amesema Kimonga.

Anasema kuwa kuishi bila mwenza ni hatari zaidi na ndiyo sababu watu wanaoishi hivyo hufa mapema kutokana na kuwa kwenye hatari ya maambukizi ya maradhi hasa ya zinaa na Ukimwi kwa vile huwa huru kujihusisha kwenye uhusiano usio salama. 

No comments:

Post a Comment