Thursday, 3 April 2014

Sheikh Abubakar Makaburi auawa kwa kupigwa risasa Mombasa

Nairobi. Sheikh Abubakar Shariff ‘Makaburi’ anayehusishwa na matukio ya kigaidi nchini Kenya ameuawa jana na watu wasiojulikana mjini Mombasa.
Sheikh huyo alimiminiwa risasi wakati akiwa katika Gereza la Shimo La Tewa mjini Mombasa jana jioni wakati akisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu dhamana kabla ya kuahirishwa kesi yake katika Mahakama ya Shanzu.
Katika tukio hilo, pia mwanafunzi wa chuo aliyetambuliwa kwa jina la Hassih Bayeko aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Walioshuhudia tukio hilo walisema mauaji hayo yalifanywa na watu waliokuwa katikagari jeusi kabla ya kutoweka. Sheikh Makaburi alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kuwa mwanachama wa kundi ugaidi la Al Shabaab, lakini alikana madai hayo.
Pia Sheikh Makaburi alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kuwaajiri vijana na kuwaingiza katika Kundi la Al Shabaab madai ambayo nayo aliyakana.
Sheikh Makaburi anakuwa muhubiri mkubwa wa tatu kuuawa kwa risasi nchini Kenya ndani ya miaka miwili . Oktoba mwaka jana, mhubiri mwingine Ibrahim Omar aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akitokea kuhubiri.
Pia Julai 2012, Sheikh Aboud Rogo aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye gari. Polisi wameimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mjini Mombasa, huku kukiwa na wasiwasi wa kuzuka kwa vurugu kutokana na mauaji ya Sheikh Kaburi.
Hata hivyo, hadi jana jioni hakukuwa na taarifa zozote za kuzuka vurugu licha ya kwamba hali ya jumla ya mji huo ilikuwa tete.
Taarifa nyingine zilisema kuwa polisi ililazimika kufyatua risasi hewani nje ya kituo cha polisi ambacho mwili wa Makaburi ulipelekwa.
Askari zaidi wametumwa katika mji huo kuimarisha usalama na Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza ilitahadharisha kuwa hali ni tete mjini humo.
chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment