Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeanza kuwapiga msasa wanasheria na maofisa ulinzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kupeleleza, kufungua na kuendesha mashtaka, ikiwa ni mkakati wa TPA kukabiliana na uhalifu bandarini.
Akifungua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mashtaka, (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, alisema yana lengo la kuwajengea uwezo maofisa hao ili wawe na uelewa wa sheria katika kuandaa mashtaka kwa makosa ya jinai yanayotokea bandarini.
Dk. Feleshi alisema TPA inatakiwa kuhakikisha inakuwa na wanasheria wa kutosha na wenye uwezo ili kupunguza tatizo la kesi za jinai.
“Ulinzi wa bandari lazima uimarishwe kwa kuweka mitambo maalumu itakayosaidia kutambua mizigo inayoingia na kutoka kwa lengo la kubaini na kutokomeza uhalifu unaoweza kutokea.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa na ofisi yake kwa kuzingatia mwongozo maalumu wa mwaka 2008 kifungu cha sheria ya mashitaka namba 18 na Ibara ya 59 B3.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TPA,Kokutulage Kazaura, alisema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa wanasheria na maofisa wa ulinzi wa TPA kwa kuwa yatawajengea uwezo wa kuendesha kesi za jinai pasipo kufuata mfumo wa zamani.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment