ujumbe mfupi wa simu uliotumwa kwako kwa makosa, kumbe mlengwa alikuwa ni mtu mwingine. Je, hii imewahi kutokea kwako?
Ujio wa simu za kiganjani imekuwa ni faraja kubwa katika kurahisisha mawasiliano kati ya mtu na mtu. Lakini pia katika kuwasiliana huku japokuwa ni manufaa, pia kumezua balaa kulikosababisha hata ndoa kusambaratika kama siyo kuvunjikia mbali.
Simu hizi wengine ambao sijui tuwaiteje, wamechukulia kama silaha ya kufanyia maasi na kibaya zaidi zimewapandikiza ibilisi wa uwongo hata kuliona jambo hilo ni la kawaida. Kumbuka uongo ni dhambi na ni moja ya amri kumi za Mungu isemayo; ‘usimshuhudie jirani yako uwongo’.
Mtu utamuuliza uko wapi muda huu? Atakujibu niko Ubungo wakati yuko Gongo Lamboto. Atakwambia yuko nyumbani kumbe yuko mahali anafanya maasi fulani. Ili mradi tu anajua kwa hakika kwamba huwezi kujua wala kufika pale alipo kwa muda ule.
Simu kwa baadhi ya watu zimewafundisha kutenda dhambi ambazo walikuwa hawazitendi hapo awali. Simu watu wengine wanazitumia kulipiza visasi. Hapo mwanzoni kabla mamlaka ya mawasiliano haidhibiti mienendo kama hiyo, hali ilikuwa tete.
Lakini sasa angalau upo utulivu hasa baada ya mamlaka hiyo kuweka bayana kuwa atakayetumtukana mwenzie kupitia simu ni rahisi kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Hata hivyo, bado simu zinatumiwa na baadhi ya wahalifu kuteka nyara watu na kwenda kuwaumiza. Mfano wa karibuni ni yaliyomkuta Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (Cuhas) mkoani Mwanza aliyetoweka muda mfupi baada ya kupigiwa simu na watu wasiojulikana.
Yupo jamaa mmoja aliyenitumia kisa chake kupitia email akielezea yaliyomkuta baada ya ujumbe toka kwa mtu asiyemjua kutumwa kupitia simu yake ya kiganjani, tena usiku akiwa na mkewe. Hebu fuatilia ujumbe wa maelezo yake kwenye email hiyo kama aliyoileta kwangu;-
Anasema hivi;-Simu yangu iko hewani masaa yote kutokana na ukweli kwamba unapomiliki simu unampa nafasi mtu yeyote akutafute ili uweze kumsaidia. Iwe kwa ushauri, fedha, maelezo na kadhalika.
Lakini pia unapokuwa na simu ujue kuwa umefunga mkataba na jamii kuwa wewe ni msaada kwa yeyote anayeuhitaji kutoka kwako saa zote.
Matumizi mabaya simu na uvumilivu mdogo wa wanajamii katika masuala ya maisha nao ni taabu kubwa. Taabu hii italeta pia usumbufu kwa familia zao na watu wengine kama ndugu, jamaa na hata marafiki.
Natoa mfano kwa kisa hiki: Siku moja yapata saa nne na nusu usiku nikiwa nimelala na mke wangu nikasikia ujumbe unaingia kwenye simu yangu.
Jioni ile, rafiki yangu mmoja alikuwa na mtoto hospitali ambaye, baada ya kumwona nikasema kimoyomoyo: Kwa hali hii huyu mgonjwa sidhani kama kutakucha.
Baada ya kusikia ujumbe, nikawaza yule mtoto amezidiwa ama vipi? Mke wangu naye akajiuliza, nani tena anatuma ujumbe usiku huu?
Nilipousoma umeandikwa hivi: “Inaonekana umetoroka Mirembe kabla hujapona, umemwacha mdogo wangu na mimba bila msaada. Huoni hali ya nyumbani? Akijifungua itakuwaje? Kweli vichaa wako wengi ”.
Niliduwaa. Mke wangu aliponiona akanyakua ile simu na kuisoma. Usiku ule ilikuwa noma, maana mke wangu alinishambulia kwa maneno makali sana. Nadhani wewe unayesoma kisa hiki unajua kuwa ungekuwa wewe ni hali gani ingekukumba.
Nilijitetea lakini sikufua dafu. Ilibidi nikae kimya na sikupata usingizi hadi kama saa kumi asubuhi. Saa kumi na mbili asubuhi, nilimpigia simu huyo dada.
Mke wangu akinisiliza kwa makini. Yule dada alijitambulisha kwa jina........ (namhifadhi na anatoka wilaya moja mkoa wa Kagera).
Aliomba msamaha sana (kwa kuwa ujumbe ulikuja kwake kwa makosa), akisema alikasirika kiasi kwamba aliona bora amtukane huyo kaka aliyempa mimba mdogo wake na kisha kutoroka akamwacha katika hali isiyoelezeka kiuchumi.
chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment