Monday 7 September 2015

Hadithi.. hadithi ... HUKUMU BILA KOSA sehemu ya 2

 

 Ilipoishia sehemu ya 1
Sikufanya kazi kama ipasavyo kwa kuwa nilijawa na msongo wa mawazo nikimuwaza mke wangu. Nilirudi nyumbani jioni bila matumaini yoyote. Bado nilikuwa katika vita kali ya kifikra,nafsi ilinisuta, ilitaka niwataarifu wazazi wa Janeth lakini moyo ulipinga.
Sasa endelea.....
Sikupenda lawama ziniangukie mimi. Nilijipa ushujaa nikiamini kuwa mimi ni mwanaume wa shoka hivyo nitajitahidi kwa hali na mali kumtafuta mke wangu bila kuwashirikisha wazazi wake wala Mama yangu. Baada ya kuoga niligeuza sebule kuwa baa. Nilikunywa pombe kali kupita kiasi mpaka usiku wa manane.
Kutokana na ulevi ilifikia hatua nikawa naongea na Janeth kimawazo kama chizi . Nilimwona amekaa kwenye sofa la mbele yangu akitabasamu kwa kuinyanyua midomo yake mipana na kuuonesha mwanya mdogo katikati ya meno yake ya mbele. “Janeth mbona unanitesa mama?Wewe mwenyewe unajua ni kiasi gani ninavyokupenda ila nashangaa unanitoroka,sijui ni kwanini?”
Niliinuka kwenda kumkumbatia.Nilijikuta nikidondoka juu ya sofa bila kusukumwa.Kumbe Janeth hayupo nipo peke yangu na pombe zangu kichwani. Nikawa mpole, mnyonge, kama kifaranga cha kuku kilichoachwa na mama yake. Machozi yalinitoka bila kujielewa.
Nilikosa raha, siku tatu tu Janeth hayupo lakini niliona ni kama mwaka mzima. Nilitamani hata atokee usiku huo. Niliapa kumsamehe Mke wangu kwa hayo aliyoyafanya ilimradi tu arudi nyumbani ili arudishe furaha yangu kama zamani. Nilimpenda sana Janeth, nilimtimizia mahitaji yote ya mwanamke ilimradi atulie na mimi. Sikutaka kumchezea na ndiyo maana toka tuanze uhusiano wetu sikuwahi kumgusa mpaka tulivyofunga ndoa.
Siyo kwamba sikuwa rijali ni kutokana na maelezo yake kuwa yeye bado kimwali na ananiandalia tunda lake kwa ajili ya zawadi ya ndoa yetu. Nilikubaliana na yote nikiamini kuwa tukiwa ndani ya ndoa tutafurahia maisha zaidi. Pia nilitaka kumhakikishia Janeth kuwa nampenda na nipo tayari kwa lolote analolihitaji ilimradi liwe ndani ya uwezo wangu.
Mipango ya Harusi ilianza na hiyo ni baada ya kumaliza chuo Kikuu. Mimi tayari nilishaanza kujihusisha na masuala ya biashara toka kitambo.Kabla ya kufunga ndoa kulitokea vikwazo vya hapa na pale toka kwa wazazi wake Janeth.
Tatizo ilikuwa ni kabila, Janeth ni mchaga na mimi ni Mmakonde. Nashangaa sana ni kwanini watu wengi wanalidharau kabila letu sijui kwa kuwa tunatokea mikoa ambayo ni Lindi na Mtwara. Watu wengine wanasema sisi siyo Watanzania ni wavamiaji toka Msumbiji.
Katika nchi yetu ya Kitanzania toka zamani Mwalimu Nyerere aliondoa suala la ukabila nchini lakini mpaka leo bado kuna baadhi ya watu wanashikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati. Janeth alinipenda sana hivyo alishikilia msimamo wake wa kuolewa na mimi siyo mtu mwingine yeyote.Alikuwa tayari kugombana na wazazi pamoja na ndugu zake kwa ajili yangu.
Alikumbuka mapenzi yetu yalipoanzia toka shuleni. Tulipendana mno mara tu tulipokutana katika shule moja hivi ya sekondari na High School iliyopo Kimara Bonyokwa wote tukiwa wahamiaji . Janeth alitokea St.Benedict iliyopo Songea na mimi nikitokea St. Mary’s Mbezi Beach hapa hapa Dar es Salaam.
Janeth alikuwa kidato cha nne na mimi nilikuwa kidato cha tano . Kwa mara ya kwanza nilipomtia Janeth machoni mwili ulisisimka kutokana na uzuri aliokuwa nao. Uso wake mwembamba kama Wanyarwanda. Mtoto alijawa na rangi ya kipekee si mweupe wala si mweusi, ni maji ya kunde.
Alikuwa na macho yaliyopambwa na kope zenye uweusi uliokolea. Nyusi zilizojaa vizuri wala hakuhitaji kutinda. Hakuwahi kununa hata kama amekasirika, muda wote alitabasamu tu.
Hakujazia sana lakini alikuwa mrefu wa wastani,kila mtu alimshauri ashiriki mashindano ya umissi wakiamini kuwa ana vigezo vya kutosha hata kumpa taji hilo. Nijitahidi kuanzisha naye mazoea taratibu taratibu kwa shida. Alikuwa msichana mpole sana, asiyekuwa na skendo yoyote mbaya tofauti na wengine ambao kila kukicha walipigania mabwana badala ya kufanya kilichowapeleka shule.
Baada ya kusikia story zake nilianza kujipanga jinsi gani ya kumwingia. Kwa jinsi alivyokuwa serious na masomo iliniwiya vigumu kumtongoza. Mawazo yalinitawala nikijiuliza ni lini nitampata Janeth ili awe wangu. Katika uhamiaji wetu pale shuleni yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika. Aliripoti shule mwezi January wakati mimi nilifika April.
Hivyo basi mwenzangu alikuwa mwenyeji kidogo tofauti na mimi.; Tulikuwa tukipata nafasi kukutana na kubadilishana mawazo ya hapa na pale kuhusiana na masomo. Sikuwahi kumweleza kitu chochote juu ya hisia zangu kwake zaidi ya kumpa sifa kwa jinsi alivyokuwa mzuri. Nilimwomba Mungu japokuwa ilikuwa dua ya kipumbavu lakini niliamini kuwa atanisaidia.
Mizizi ya mapenzi ilichipua na kumea ndani ya moyo wangu. Wanafunzi mbalimbali wa kiume walimtongoza lakini mwisho wake wakaishia kupigwa chaga yaani walikataliwa.Kitendo cha Janeth kuwakataa wanafunzi mbalimbali kiliwakasirisha na kuamua kuanzisha bifu na mimi wakiamini kuwa eti mimi ndiyo namshauri awakatae.
Kiukweli sikupenda ugomvi na wanafunzi wenzangu. Niliishi nao kistaarabu na kwa amani zaidi. Kila aliyekuwa adui wangu nilimpenda na marafiki zangu niliwapenda zaidi, Janeth alianza kuonesha dalili za Mapenzi kwangu. Siku zote penzi ni kikohozi kulificha huliwezi. “Body language was take place”
Alianza kuniletea zawadi mbalimbali,asiponiona siku nzima alikosa raha. Mara kwa mara kwenye disco la shule alipendelea tucheze pamoja. Nilipomshika kiuno nilihisi shoti na aliponikumbatia nilipagawa zaidi. Baada ya mziki usiku sikuweza kulala.
Niliwaza na kuwazua vitendo alivyonifanyia Janeth wakati wa muziki. Nilipata ujasiri wa kumweleza ya moyoni mwangu.Nilitaka atambue kuwa nampenda si masihara. Ilikuwa mwezi wa tano mwishoni. Tulikuwa katika maandalizi ya mitihani ya kufunga shule. Hilo lilinipa kikwazo kidogo
Muda mwingi tulikuwa bussy tunasoma kwa ajili ya mitihani. Mawasiliano yalizidi kupungua kadri siku zilivyozidi kwenda. Kila mtu alijichimbia kwenye darasa lake. Tulionana siku moja moja sana. Mpaka siku tunayoanza mitihani sikufanikiwa kumweleza Janeth kitu chochote.Siku tuliyomaliza mitihani ndiyo siku ya kufunga shule. Nilimtafuta kila kona, hatimaye nikampata.
Nilikuwa nahitaji kitu kimoja tu kutoka kwake. Si kingine bali namba za simu. Alinipa bila hiyana. Tuliagana kila mmoja akimtakia mwenzake likizo njema. Alifuatwa na mama yake, baada ya taratibu zote za kufunga shule kukamilika alingia ndani ya gari la mama yake na kuondoka. Jioni na mimi nilirudi nyumbani Mwananyamala.
Tukiwa likizo nilimpigia simu mara kwa mara hatimaye siku hiyo nikakata shauri “Leo lazima nimwambie, nitakuwa kimya hivi mpaka lini?”Nilinunua vocha ya kutosha na kuweka kwenye simu. Nilibofya namba zake na kupiga. Niliweka sikioni kusikiliza, ilipoanza kuita tu mapigo yangu ya moyo yakaongezeka.
Uoga ukaniingia, midomo ikatetemeka nikitafakari nianzeje kumweleza ukweli punde tu atakapokea simu. Simu iliita mpaka ikakata. Nikamua kupiga tena. Safari hii haikuchukua muda mara ikapokelewa “Hello ! Japhet mambo vipi?”Sauti nyororo tamu kama asali ilinisalimia upande wa pili.
MTUNZI: FREDY MZIRAY

No comments:

Post a Comment