HOFU imetanda kwa wananchi wa kata ya Tungi eneo la Nane Nane mkoani Morogoro, kutokana na kuibuka kwa kundi la mbwa wala watu ambao wameshaua mkazi wa eneo hilo, Paulina Mathias (75-80), na kumjeruhi mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, mwenyekiti wa mta wa Tungi, Aidani Konja, alisema bibi huyo anasadikiwa kukamatwa na kundi la mbwa na kuburuzwa hadi katikati ya mikonge na kuanza kuliwa.
“Tulipofika eneo alipoliwa mita kama 500 kutoka njiani, mwili wa marehemu ulikuwa umenyofolewa nyama takriban zote mguuni na mikononi kasoro tumbo ambalo alikuwa amejifunga nguo,” alieleza mwenyekiti huyo.
Alisema inawezekana bibi huyo alikuwa akitokea mtaa wa jirani wa Mfaranyaki kuelekea kwenye makambi ya mkonge na ndipo alipokutana na mbwa hao ambao walimshambulia.
Mbali na bibi huyo, mbwa hao wanaosadikiwa kuwa na njaa, walimjeruhi Ismaili Abdallah (24) kwa kumshambulia kabla ya kuokolewa.
Aidha, diwani wa kata hiyo, Daudi Mbao, akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana wakati wa zoezi la kuwasaka mbwa hao, alisema wamefanikiwa kuwaua mbwa wawili kati ya sita na kusema wamezua hofu kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.
Alisema miili ya mbwa waliouawa imechukuliwa na maofisa wanyamapori na maofisa afya, ili kubaini ni aina gani ya mbwa na kama wanakabiliwa na kichaa cha mbwa.
Alifafanua kuwa wameshangazwa na aina ya mbwa hao ambao wameibuka ghafla na kushambulia watu, jambo ambalo limewajenga hofu wananchi wa kata hiyo na kulazimika kuwazuia watoto wao kwenda shule baada ya juzi mbwa hao kuvamia baadhi ya shule za kata hiyo.
Naye mkazi wa kata hiyo, Mussa Chabruma, alisema zoezi la kuwasaka mbwa lilikuwa gumu kutokana na kushindwa kupata msaada wa haraka kutoka askari wa wanyama pori ambapo walilazimika kutumia silaha za jadi kuingia porini kuwasaka mbwa hao.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tungi, Pili Mamboka, alisema zoezi la kuwasaka mbwa hao linaendelea ili kuhakikisha hofu iliyotanda kwa wananchi wa kata hiyo inaondoka.
No comments:
Post a Comment