IMEBAINIKA kuwa migogoro mingi ya ardhi inayotokea katika Manispaa ya Kinondoni na jiji la Dar s Salaam kwa ujumla inasababishwa na watu ambao sio raia kuvamia maeneo yasiyoendelezwa na kuyauza kwa watu wengine.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dares Salaam Said Mecky Sadik alipozungumza na waandishi wa habari juu ya uvamizi wa mashamba wilayani Kinondoni.
Sadik alisema migogoro iliyopo katika Manispaa hiyo ni tofauti na migogoro mingine iliyozoeleka katika jamii kwani katika migogoro hii yapo makundi ya watu wanajikusanya hadi kufikia 50 na kwenda kuvamia eneo lililo wazi kisha kugawana maeneo hayo.
“Hawa watu wakishavamia hujipanga kujilinda kwa kufuatilia nyendo za watu walio wageni na makundi yao na wakishabaini mgeni hasa kama ni mmiliki wa eneo husika watu hawa hujikusanya kwa kupiga filimbi kisha kwenda kumshambulia muhusika, hili halikubaliki kwani serikali ipo na itawashughulikia,” alisema.
Aliyataja maeneo yaliyoathirika na uvamizi huo kwa wilaya ya Kinondoni ni kata ya Wazo, Mabwepande, mitaa ya Kilimahewa, Mivumoni, Nakasangwe, Madale na Bunju.
Ameongeza kuwa uchunguzi uliofanywa na serikali umebaini wavamizi hao hawajengi makazi ya kudumu na huharibu mali za wenyeji walizozikuta katika maeneo waliyovamia na kujianzishia utawala wao.
Alisema watu walio ndani ya mita 500 kutoka kambi za jeshi wabomoe wenyewe kuanzia sasa na waliovamia maeneo ya watu aliiagiza manispaa ya Kinondoni kulishughulikia kwa haraka suala hilo.
Hata hivyo Sadik alishindwa kubainisha hatua watakazochukuliwa watendaji waliosababisha watu kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa kusema hilo litafuata taratibu na watakaobaionika watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment