SHIRIKA lisilo la kiserikali la Under The Same Sun (UTSS) limesema halina uwezo wa kifedha au rasilimali za kuwafadhili Watanzania wote wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Kauli hiyo ya UTSS imekuja baada ya kupokea maombi mengi ya albino wanaotaka kusaidiwa matibabu ya saratani na magonjwa mengine, kujikimu kimaisha, kulipa kodi za nyumba, kujengewa nyumba na kufadhiliwa miradi ya kiuchumi.
Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana kwa vyombo ya habari na Meneja Uendeshaji wa UTSS, Gamariel Mboya, ilieleza kuwa jukumu la kutoa huduma za afya, elimu na nyingine za kijamii kwa Watanzania wote limo mikononi mwa serikali.
“Serikali ya Tanzania imeshawahi kutangaza kupitia viongozi wake mbalimbali kwamba unatoa huduma za afyya bila malipo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi…hii ni pamoja na saratani ya ngozi.
“Shirika linatoa rai kwa viongozi wa serikali kutimiza ahadi hiyo na kuyanusuru maisha ya wananchi wake wenye ulemavu wa ngozi ambao hapa nchini wanafariki dunia kabla ya kufikia umri wa miaka 30,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, UTSS imeishauri serikali kuingiza nchini mafuta ya kujikinga na miozi ya jua katika orodha ya dawa zake ili zisambazwe kwa wingi na ziwafikie kwa urahisi albino.
No comments:
Post a Comment