Thursday, 15 December 2011

SAKATA LA POSHO ZA WABUNGE Makinda ang'olewa madarakani

HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kusita kutia saini waraka wa kuidhinisha nyongeza ya posho za wabunge, imemjengea chuki Spika wa Bunge, Anne Makinda, mbele ya umma, huku taarifa mpya zikieleza kuwa lilikuwa ni jaribio la pamoja la wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, kufanya kile wanachokiita ‘kuboresha mazingira ya kazi.’
Wiki iliyopita Makinda alitoa tamko kwamba posho ya vikao vya wabunge (sitting allowance), imeongezwa kutoka sh 70,000 ya sasa hadi kufikia sh 200,000 kwa siku, akidai kuwa hatua hiyo inalenga kuwanusuru wabunge na kuwawezesha kutimiza wajibu wao vizuri, kwani wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha hususan wawapo mjini Dodoma.
Hata hivyo, wakati Makinda anatoa tamko hilo, Rais Kikwete alikuwa bado hajasaini waraka husika wa kuidhinisha nyongeza hiyo, kitendo kilichotafsiriwa na wadadisi wa mambo kuwa kililenga kupima joto la wananchi kwanza kabla rais hajafikia uamuzi wa mwisho wa kusaini.
Rais Kikwete amewahi kusikika mara kadhaa akizungumzia haja ya kuboreshwa kwa masilahi ya wabunge, mara moja ikiwa ni mwaka 2006 wakati akizindua jengo jipya la Bunge, ambapo pamoja na mambo mengine, alisikika akisema:
Serikali kwa upande wake itaendelea kuchangia juhudi za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi zenu hapa bungeni na majimboni. Tutafanya kila kinachowezekana, kulingana na uwezo uliopo, kuwapatia mahitaji ya kuwawezesha kuwa wabunge wazuri kwa wapiga kura wenu.”
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameieleza Tanzania Daima Jumatano kuwa kamwe Spika Makinda asingeweza kusukuma mpango huo peke yake bila kuwa amehakikishiwa ridhaa ya rais, ambaye kisheria ndiye mwenye mamlaka ya kupandisha posho hizo.
Kwamba hata Tume ya Huduma za Bunge isingeweza kuwasilisha kwa rais pendekezo la kupandishwa kwa posho hizo, bila kupewa uwezekano wa kukubaliwa na mkuu huyo wa nchi.
Wameeleza kwa muda mrefu sasa suala la nyongeza ya posho, mishahara na masilahi yote ya wabunge kwa ujumla wake, limekuwa ni ajenda ya pamoja ya wabunge wa CCM na serikali yake, hivyo hatua ya Makinda kuachwa akishambuliwa peke yake imetokana tu na rais kurudi nyuma kwa sababu ya kuhofia kile kinachodaiwa kuwa  ni ‘nguvu ya umma.’
Wamefafanua kuwa hata Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alipokuwa akipinga mishahara mikubwa ya wabunge katika Bunge lililopita, wabunge wa CCM na serikali ya Kikwete waliungana kuitetea.
“Hili si kosa la Makinda...Rais alikuwa tayari kusaini waraka huo wa posho, lakini sasa amesita kufanya hivyo baada ya mpango huo kupingwa sana na umma”, alithibitisha mjumbe mmoja aliyehudhuria kikao cha Tume ya Huduma za Bunge, iliyowasilisha pendekezo hilo kwa rais.
Aidha, hatua ya  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kutoa tamko la kupinga nyongeza ya posho, imetafsiriwa kuwa ni ya kujaribu kujinasua dakika za mwisho kutoka kwenye hasira za umma, hasa baada ya kile alichokitanguliza Makinda kupata upinzani mkali.
Wakati Makinda ikielezwa kuwa alifanywa chambo na jaribio hilo kukwama kwa rais ‘kuogopa’ kuidhinisha posho, tayari gazeti hili limenasa mipango ya siri ya wabaya wake wanaojipanga kulitumia suala hilo kujenga hoja ya kuonyesha udhaifu wake, ili hatimaye ang’oke kwenye wadhifa huo.
Kundi la wabaya hao linatajwa kuwa ni lile lililokuwa likimuunga mkono zaidi Spika aliyepita, Samuel Sitta, ambalo linadaiwa kuandaa hoja ya kutokuwa na imani na Spika, kwa lengo la kuiwasilisha katika kikao kijacho cha Bunge, mwezi Januari mwakani.
“Posho hii haijaruhusiwa na rais, licha ya kulipwa kutoka mfuko wa Ofisi ya Spika. Ombi la kupandisha lilishapelekwa Ikulu, lakini wino wa mkubwa haukuwa umeshamwagwa. Spika kajinyakulia mamlaka ambayo hana kwa kujua udhaifu wa JK. Mambo yote ya fedha yako mikononi mwa Katibu wa Bunge,” alisema mmoja wa wabunge hao wa CCM.
Hadi sasa Katibu wa Bunge, Kashilila  ambaye alikuwa Uingereza wakati Spika anatangaza nyongeza hiyo ya posho, amesikika akisisitiza kuwa posho mpya hazina ruksa ya mamlaka husika.
Mbali na suala la nyongeza ya posho watakalolitumia kuthibitisha udhaifu wa Makinda na jinsi asivyostahili  kuendelea kuongoza chombo hicho nyeti nchini, taarifa zaidi zinasema wabunge hao pia wana chuki zao binafsi dhidi ya mama huyo, kwa madai kuwa amekuwa akiwanyima fursa ya kusafiri nje ya nchi kwa shughuli za kibunge.

No comments:

Post a Comment