Jamhuri wakopa kwenda Zimbabwe
MSAFARA wa wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Jamhuri, umeondoka visiwani hapa kwenda Zimbabwe tayari kwa mechi ya marudiano dhidi ya Hwange FC ya huko.
Ukiwa na watu 25 wakiwemo wachezaji na viongozi, msafara huo uliondoka ukiwa na matumaini ya kufanya vyema licha ya kukutana na kipigo cha mabao 3-0 katika mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba.
Pambano hilo linatarajiwa kupigwa Jumapili katika jimbo la Mathebeleland, huku Jamhuri ikilazimika kushinda kwa mabao 4-0 ili iweze kusonga mbele.
Pamoja na matumaini hayo madogo ya kufanya vyema, uongozi wa Jamhuri ulielezea kusikitishwa na mazingira magumu ya upungufu wa nauli hali iliyowalazimisha kukopa kiasi cha dola za Marekani 12,000 kwa wahisani ili kuweza kusafiri.
Abdallah Abeid ‘Elisha’, alisema, awali walikuwa wakitarajia kupata ufadhili, lakini hawakuweza kufanikiwa kupata msaada wowote kama walivyokuwa wakitarajia.
Meneja huyo, alisema timu yake ilikuwa na akiba ya dola 6,000 pekee ambazo zingelitosha kuisafirisha kwa basi hadi Zimbabwe, lakini iliamua kuchukua dhamana ya kukopa dola nyengine 12,000 ili kukamilisha mahitaji ya dola 18,000 zilizokuwa zikihitajika, huku wakipata msaada wa tiketi moja kutoka Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
“Tunakabiliwa na kibarua kigumu, lakini mchezo wa soka ni dakika 90, chochote kinaweza kutokea,” alieleza Elisha.
No comments:
Post a Comment