NA MWANDISHI WETU
SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF), limesema litamchukulia hatua za kisheria mtu atakayebainika kuuza cd za shughuli za maziko za marehemu Steven Kanumba bila ridhaa ya familia.
Tamko hilo lilitolewa jana na Rais wa TAFF, Simon Mwakifamba nyumbani kwa marehemu, Sinza Vatican mbele ya familia ya marehemu, akisema hilo litafanyika kwa idhini ya familia hiyo.
Mwakifamba alisema tayari wameshapata taarifa za watu kuanza kuuza cd hizo kwa lengo la kujipatia fedha jambo ambalo sheria ya filamu hairuhusu.
Kwa mujibu wa rais huyo, marufuku hiyo inatokana na Kanumba alikuwa akitegemewa na familia yake kupitia kazi za filamu, hivyo bila kuwepo kwa usimamizi mzuri wa kazi hizo, familia itayumba.
Alisema kama cd hizo zitasimamiwa vizuri pato, lake litaingia kwenye familia na kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku badala ya jasho hilo kufaidiwa na watu wengine wasiohusika.
Kupitia mkutano huo, kwa niaba ya familia Mwakifamba alitoa shukrani kwa wote waliojitokeza katika mazishi ya Kanumba huku akisema, TAFF itamkumbuka kwa mengi.
Alisema, mbali ya uwanachama wake Kinondoni, pia alikuwa mjumbe wa kamati ya TAFF ya kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya kanuni ya sheria za filamu za mwaka 2011.
Aidha, alisema kuwa, Kanumba alikuwa ni kati ya wafadhili wa Shirikisho hilo na akitoa mchango mkubwa katika kuleta umoja na mapinduzi ya kweli katika tasnia ya filamu.
CHANZO CHA HABARI HIZI NI GAZETI LA SAYARI
No comments:
Post a Comment