NA ANDREW CHALE
WAKATI taifa likiwa bado linaomboleza msiba mzito wa msanii mahiri wa filamu, Steven Kanumba aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita na kuzikwa Jumanne wiki hii, wajanja wametengeneza kitabu cha maisha yake na kukiuza bila idhini ya familia yake.
Kitabu hicho chenye picha ya msanii huyo, kilionekana jana katika maeneo ya Ubungo, na kimekuwa kikinunuliwa kwa kasi kubwa chini ya jina la ‘Historia na Maisha ya ‘The Great’ Steven Kanumba.’
Kava la kitabu hicho lina picha kubwa ya marehemu Kanumba.
Baadhi ya watu waliozungumza na Sayari jana, walionesha kusikitishwa kwao na kitendo hicho kwa sababu sio tu ni dhuluma kubwa dhidi ya familia ya marehemu, pia dhuluma hiyo kufanywa wakati familia, ndugu na jamaa za marehemu bado wakiwa na majonzi makubwa.
Wadau hao wamekwenda mbali zaidi wakisema, vitendo hivyo vinapaswa kukemewa na jamii kwa kutonunua kazi hizo haramu kwa mujibu wa sheria ya hakimiliki.
“Binadamu hawana utu… hata matanga hawajaanua watu wameshaanza kujinufaisha na mali za marehemu… huu ni wizi wa mchana kweupe, serikali ichukue hatua dhidi ya wahusika kwa kuwakamata,” alisema Lily Kitulya kupitia moja ya mitandao ya kijamii.
CHANZO CHA HABARI HIZI NI KUTOKA KATIKA GAZETI LA SAYARI.
No comments:
Post a Comment