Friday, 20 April 2012

KIJIJI CHA TAMBUA HAKI Wosia wa Kanumba kwa Watendaji Serikali za Mitaa


HABARI za leo ndugu msomaji wa safu hii ya Filamu za Kwetu. Ni matumaini yangu u-bukheri wa afya na unaendelea vema na kazi ya ujenzi wa taifa. Tunakutana katika kiwanja hiki tukiwa bado na simanzi ya kuondokewa na msanii mahiri wa tasnia hii, Steven Kanumba.
Katika kumuenzi msanii huyu, nitakuwa nikiwaletea mfululizo wa baadhi ya filamu zake alizozicheza kabla ya umauti kumfika usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7.
Kwa kuanza, leo nakuja na ‘Kijiji cha Tambua Haki’, filamu yake ya mwisho iliyokuwa sokoni.
Filamu hii hadithi yake imetungwa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utoaji elimu ya uraia kwa wananchi (Policy Forum) na kuendelezwa na Mayasa Mrisho.
Wahusika wakuu katika filamu hii, ni Kanumba, Masanja Kajala, Mayasa Mrisho, Bakari Makuka ‘Beka’, Mohamed Fungafunga ‘Jengua’, Abdallah Mkumbila na Novatus Mayanja ‘Nova’. 
Katika filamu hii tunamuona Kanumba akiwa askari mgambo wa kijiji akiongozwa na bosi wake Jengua ambaye kutokana na cheo, akawa anayatumia vibaya madaraka.
Suala hilo halikumpendeza Kanumba kwa kuwa alikuwa akiona waziwazi jinsi wananchi walivyoonewa, ikiwemo kunyang’anywa mali zao na wengine kufikia hatua ya kupigwa bila sababu.
Kama haitoshi, Kanumba alikuwa akishuhudia namna viongozi wake walivyokuwa wakitafuna fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijiji chao. Hivyo anaamua kuvua magwanda  na kuwa mwananchi wa kawaida.
Hata hivyo, hatua hiyo haikuwafurahisha viongozi hao wa Serikali ya Mtaa kwani walikuwa wakijua wazi siri zote ambazo Kanumba alikuwa akizijua, zitafika kwa wengine, ngazi za juu.
Kwa mazingira hayo, walianza kumfanyia visa ilimradi tu ahame mtaani hapo, wakianza kumuua mwanae wa pekee.
Zaidi ya hapo, walitaka kumchomea nyumba hadi kukimbilia msituni na mke wake ambaye naye kutokana na mshtuko wa moyo, alifariki.
Mwisho, Mkuu wa Wilaya anaenda kukagua miradi ya kijiji hicho, ikiwemo kusikiliza kero za wananchi, ndipo anashuhudia madudu ambayo watendaji wake wamekuwa wakifanya kwa kutokamilisha miradi huku wananchi wakilalamika.
Baada ya Mkuu wa Wilaya huyo wa wilaya kupata malalamiko hayo, anaamuru viongozi hao wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria

       CHANZO CHA HABARI GAZETI LA SAYARI

No comments:

Post a Comment