Monday 16 April 2012

LULU ATISHIA!!!!


MSANII Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayeshikiliwa mahabusu ya Seregea, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji ya msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Kanumba, amedaiwa kutishia kujiua. 
Habari za uhakika kutoka gerezani hapo, zinasema Lulu alikuwa kwenye hali hiyo siku tatu za kwanza tangu alifikishwe hapo.
Shitaka linalomkabili Lulu, ni tuhuma za mauaji ya Kanumba aliyefariki usiku wa kuamkia Aprili 7, baada ya kupoteza fahamu nyumbani kwake Sinza Vatican, Kinondoni, Dar es Salaam.
Baada ya kusomewa mashtaka kwenye Mahakama ya Kisutu na kutakiwa kurudi hapo Aprili 23, alipelekwa Segerea.
Akiwa huko, amekutana na msanii mwenzake Kajala Masanja anayekabiliwa na tuhuma za kutakatisha fedha haramu pamoja na mumewe Faraja Augustino.
Habari kutoka gerezani hapo na kuthibitishwa na ofisa ambaye hakutaka kutajwa jina, zinasema siku tatu za kwanza zilikuwa ngumu sana kwa Lulu, ingawa taratibu ameanza kuzoea mazingira.
Chanzo hicho kinasema, hatua ya Lulu kugoma kula chakula cha gerezani hapo, haikuwa tatizo sana, anakula chakula kutoka nje kutokana na uwezo wa ndugu zake.
Hata hivyo, kikadokeza kuna uwezekano mkubwa wa Lulu kubadili msimamo huo pale ndugu watakapochoka kupeleka chakula na yeye kuzoea hali ya gerezani.
Lakini, visa vingine vya Lulu kwa siku za kwanza gerezani hapo, ni kuonekana kama mtu anayeweweseka na kutishia kujiua.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, Lulu alikuwa kwenye hali hiyo siku tatu za kwanza, hivyo kuwapa askari kazi ya ziada kuhakikisha usalama wake.
Yaelezwa, ndio kisa cha kumkabidhi kwa Kajala kwa lengo la uangalizi wa karibu zaidi na kumfariji kwa vile ni msanii mwenzake.
Mbali ya Kajala kumzidi umri Lulu, pia amekuwepo gerezani hapo kwa muda sasa, kiasi cha walau anayajua mazingira.
Habari zaidi zinasema kuwa, tangu Lulu apelekwe hapo, wageni wengi wamekuwa wakimiminika kumjulia hali hadi kuwa kero.
Chanzo cha uhakika kutoka gerezani hapo, kimedokeza, wingi huo ukiongozwa na wasanii, umesababisha watu kupigwa marufuku kumuona msanii huyo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, licha ya marufuku hiyo, kilichofanyika ni kupungua tu kwa watu wa kumuona msanii huyo.
“Tangu Lulu aletwe hapa (Segerea), kila siku tukawa tukipokea watu wengi hasa wasanii waliokuja kumwona, hadi kuwa kero,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema kuwa, sababu hasa ya kuzuia wingi wa watu kufika gerezani hapo kumwona Lulu, ni kuepusha usumbufu kwa askari waliokuwa wakikosa muda wa kufanya kazi nyingine.
“Ilikuwa kero tupu…watu, hasa wasanii wenzake walikuwa wakimiminika kila siku kumjulia hali Lulu, hadi tunaona hapana, kwani ilikuwa ikizuia hata kufanya shughuli nyingine,” kilidokeza chanzo hicho.
“Karibia kila mgeni, Lulu…Lulu, Lulu, hadi ilikuwa inachosha, ilikuwa ikituzuia kufanya kazi nyingine, kwa sasa bado wanakuja, lakini wamepungua sana sasa.”  
Sayari ilipomtafuta Msemaji Mkuu wa Jeshi la Magereza, Omari Mtiga, alisema kuhusu msanii huyo kutishia kujiua, hana taarifa hizo kwani alikuwa safarini.
“Nimerudi jana (juzi) kutoka safari… sijui lolote; labda niulize kwa wenzangu, nikupe jibu sahihi.
“Lakini hilo la kuweweseka,ni jambo la kawaida ambalo huwapata watuhumiwa wengi,” alisema Mtiga ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza.
             
                                   CHANZO CHA HABARI HIZI KUTOKA GAZETI LA SAYARI.

No comments:

Post a Comment