HARAKATI za Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi katika kuisaidia jamii na ushiriki wake katika mapambano dhidi ya ufisadi, zimemuwezesha kutunukiwa tuzo mbili za Umoja wa Mataifa (UN).
Katika sherehe hizo zilizofanyika Dar es Salaam jana, Mengi alitunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Mwaka 2010 ya Uongozi na Kujali Utu na ya Mafanikio ya Asasi Binafsi za Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2010-2011.
Utambuzi wa kumteua Mengi kuwa mshindi wa tuzo hizo mbili, ulifanywa chini ya uratibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Global 2000 (2010) chini ya usimamizi wa Mkuu wa taasisi hiyo, Dk. William Morris. UN iliwakilishwa na Mratibu Mwakilishi wa UN nchini, Alberic Kacou; na sherehe hizo kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa akiwamo mgeni rasmi Jaji Mkuu, Mohammed Chande.
Akizungumzia mchakato wa kumuibua Mengi kuwa mshindi, Dk. Morris alisema taasisi hiyo ilifuatilia na kuridhishwa na harakati za mfanyabiashara katika kuwasaidia watu wasiojiweza kama watu wenye ulemavu, yatima na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Alisema licha ya kuhifadhi mazingira, lakini pia harakati zake katika kukabiliana na ufisadi na hasa alipowataja hadharani watu aliodai wanajihusisha na ufisadi ili kulisaidia Taifa lake kukabiliana na vitendo hivyo.
Alisema pamoja na kupambanishwa na washindani wengine wengi wenye sifa katika kuitumikia jamii, Mengi alishinda kwa asilimia zaidi ya 80, ikiwa ni mara ya kwanza kutokea tangu UN ilipoanza kutoa tuzo hizo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi Tuzo ya Uongozi na Kujali Utu, Kacou alisema UN imempa tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika kuisaidia jamii si tu Tanzania na Afrika, bali duniani kote kwa ujumla.
Alisema UN imeridhika na harakati za Dk. Mengi akiwa mfanyabiashara binafsi katika kupambana na umasikini, kuilinda dunia, kuwasaidia masikini na hasa alipokuwa anaitumikia jamii kama Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na akiwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Kusaidia Watu Wenye Ulemavu Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mengi alisema “Nimepata heshima kubwa sana kwa kutunukiwa tuzo hizi ambazo ninazipokea kwa unyenyekevu mkubwa. Ninachukua fursa hii kuwashukuru Taasisi ya Global 2000 (2010) International kwa utambuzi huu na Dk. Morris kwa kutayarisha hafla hii.”
NA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment