MKAZI wa Magomeni Makuti mkoani Dar es Salaam, Othman Bonde (35), anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Zanzibar baada ya kukamatwa na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume wiki moja iliyopita.
Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Muhibu Juma Mshihiri alithibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na kusema taratibu zinafanyika ili kumfikisha mahakamani.
Akifafanua zaidi, Mshihiri alisema Bonde alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaan Karume akiwa katika ndege ya Shirika la Ndege la Oman Airline akitokea Sao Paul nchini Brazil.
Bonde alikamatwa uwanjani hapo baada ya kutiliwa shaka na wafanyakazi wa uwanja huo wakiwamo askari polisi, ambapo uchunguzi ulianza.
Pipi 105 zilitolewa na mtuhumiwa kwa njia ya haja kubwa wakati pipi sita zilitapikwa na mtuhumiwa. Kwa mujibu wa tiketi ya ndege ya Bonde, alikuwa akitoka Sao Paulo na kupitia Oman na kutumia ndege ya shirika hilo ambayo ilimfikisha hadi Zanzibar.
“Tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha uchunguzi na mtuhumiwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabili za kusafirisha madawa ya kulevya na kuyaingiza nchini,” alisema Mshihiri.
Hicho ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kukamatwa katika uwanja huo wa ndege kwa mwaka huu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeimarisha vifaa vya ulinzi vya kugundua dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume kwa ajili ya kudhibiti kasi ya uingizaji wa dawa hizo katika njia kuu ya uwanja wa ndege pamoja na Bandari ya Malindi.
Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupeleka mbwa ambaye hunusa na kutambua dawa za kulevya pamoja na vitu vyengine hatari ambavyo havitakiwi kuingizwa nchini.
NA HABARI YA LEO
No comments:
Post a Comment