MWANAFUNZI wa Darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Dovya, Lazack Maulid (7), mkazi wa Yombo Darajani amekufa baada ya kusombwa na maji na kuzama wakati akiokoa ndala zake aina ya ‘yeboyebo’ zilizochukuliwa na maji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, David Misime alisema mwanafunzi huyo alisombwa juzi saa 7.00 mchana wakati akicheza na wenzake kwenye mkondo wa maji yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi katika eneo la Yombo Darajani.
Alisema wakati wakiendelea na mchezo ndipo ndala moja ya mwanafunzi huyo ilichukuliwa na maji.
Aliamua kuifuata lakini kabla hajaipata alisombwa na maji hayo yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini.
Alisema maji hayo yalimzidi mwanafunzi huyo na hatimaye kunywa maji mengi na kusombwa kisha kuzama na kufa papo hapo.
Misime alisema kuwa mwili wa mtoto huyo uliopolewa na wananchi wa maeneo hayo na umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke huku polisi wakiendelea na upelelezi zaidi.
NA HABARI YA LEO
No comments:
Post a Comment