Monday, 24 November 2014

Zahanati ina muuguzi mmoja anapima, kutoa dawa na kuzalisha kwa kibatari!

Katika hali isiyo ya kawaida, zahanati ya kijiji cha Matanga, Manispaa ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, ina muuguzi mmoja tu ambaye anafanya kazi za upimaji magonjwa,  kutoa dawa na kuzalisha kinamama kwa kutumia mwanga wa kibatari.

Muuguzi huyo, Bruno Ntalyoka (40), amefanya kazi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya daktari wa zahanati hiyo kuhamishwa.

Akizungumza na mwandishi wa NIPASHE,  aliyetembelea kijiji hicho hivi karibuni,  Ntalyoka alisema pamoja na kupokea wastani wa wagonjwa 57 kwa siku, ameweza kuimudu kazi yake na anajisikia furaha kuhudumia wagonjwa wake.

Ntalyoka alisema alianza kazi hiyo mwaka 1985 katika kijiji cha jirani cha Malangani na alihamishiwa hapo miaka mitano iliyopita.

Alisema huko nyuma zahanati hiyo ilikuwa na daktari mmoja na yeye alikuwa akimsaidia, lakini baada ya kuhamishwa kazi zote anazifanya yeye.

 “Nafanya kazi vizuri tu hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi, naamini haya yote yatakwisha baada ya serikali kuleta daktari.” alisema Ntalyoka.

MAJUKUMU YA KAZI
Muuguzi huyo alisema kila siku anapofika kazini, jambo la kwanza ni kuorodhesha wagonjwa, kabla ya kwenda maabara kwa ajili ya kuchunguza matatizo yao.

“Nashukuru katika zahanati kuna darubini na vipimo vya magonjwa kama malaria na magonjwa ya zinaa, inakuwa rahisi kwangu kujua matatizo yao na aina ya tiba inayotakiwa kuwapa,” alisema.

Baada ya hatua hiyo, anakwenda katika chumba cha matibabu kwa ajili ya kutoa tiba.

“Kuna wale wanaotakiwa dawa ya kawaida lakini wapo wanahitaji sindano au upasuaji mdogo,  wote nawahudumia kwa zamu bila manung’uniko,” aliongeza.

KUZALISHA NA KIBATARI 
Hata hivyo, alisema inapojitokeza suala la mama mjamzito anataka kujifungua, inambidi kusitisha huduma zote kwa wakati huo kwa ajili ya kumhudumia.

Alisema kwa kawaida kila mwezi anazalisha kinamama 18 ambapo ni wastani wa wanawake wawili hadi watatu kwa siku.

Pia alieleza kwamba kazi hiyo inakuwa ngumu nyakati za usiku kutokana na zahanati hiyo kukosa umeme, hivyo inambidi kutumia mwanga wa taa ya kibatari kuzalishia.

Alisema kitu kingine kinachosababisha kazi yake kuwa ngumu ni uhaba wa maji,lakini amebuni njia mbadala ya kuhifadhi maji kwenye madumu ya plastiki kwa ajili ya kumsaidia.

Wakati huo huo, uongozi wa Manispaa ya Sumbawanga umempelekea muuguzi mwingine kwa lengo la kumsaidia kutoa huduma.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mathew  Sedoyeka, alikiri kuwapo kwa uhaba wa wataalamu wa afya katika wilaya yake, ila alisema wanajitahidi kukabiliana na hali hiyo kwa kuweka mgawanyo sawa kwa wafanyakazi wachache waliopo katika maeneo yote.

Alisema hali hiyo inachangiwa na ongezeko la vituo vya afya pamoja na zahanati katika vijiji mbalimbali na kwamba serikali inategemea kupata wataalam wapya watakaoziba nafasi hizo
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment