Friday 18 January 2013

MUSA KITALE: Mwananyamala imenipa ujuzi wa kuigiza ‘uteja’


MIONGONI mwa wasanii ambao kwa sasa ni gumzo kwenye fani ya uigizaji wa vichekesho, ambao ukiambiwa uwataje, ni vigumu kumruka Musa Kitale ‘Kitale’ au ‘Rais wa Mateja’.
Kitale ambaye alikuwa rafiki wa karibu zaidi na aliyekuwa mkali wa vichekesho, marehemu Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ kwa sasa anatesa na staili yake ya kuigiza kama teja na wengine kuonekana kumuiga, jina lake lilianza kuwika alipokuwa katika kundi la Kaole.
Kitale katokea wapi?
Kitale anasema, alisoma katika Shule ya Msingi Uzuri iliyopo Sinza, Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 2001. Baada ya hapo, alijiunga na Sekondari ya Morogoro na kumaliza mwaka 2006.
Anasema, japokuwa sanaa alianza rasmi alipokuwa darasa la saba, ambako alikuwa akiigiza na kundi la Kaole, lakini shughuli hii ilimkolea hasa pale alipomaliza kidato cha nne na kuamua kuhamia Kampuni ya Tuesday Entertainment, chini ya Tuesday Kihangala na jina lake likazidi kung’ara katika mchezo wa Jumba la Dhahabu, uliokuwa ukirushwa na kituo cha Star TV.
Mbali na kuigiza Jumba la Dhahabu, pia alishacheza ‘Ua Jekundi’ kama mtoto mtukutu, wakati akiwa katika Kampuni hiyo ya Tuesday na hapo ndipo staili yake ya uteja ilipompandisha chati.
Hata hivyo, Kitale kwa sasa anabainisha kuwa anafanya kazi chini ya Kampuni ya Al Rihamy, ambayo anadai kuhamia kunatokana na masilahi, kwani yeye kama binadamu wengine anataka atengeneze maisha yake ya baadaye.
Kazi za filamu

Kitale anasema pamoja na kufanya kazi na kampuni mbalimbali, pia ameweza kutengeneza filamu zake mwenyewe kama vile ‘Mbwembwe’, ‘Kubwa Jinga’ na ‘Porojo’ ambazo ni za vichekesho (comedy),’Bad Night’, na ‘More Than a Lion’ aliyomshirikishwa msanii wa miondoko ya bongo fleva, Dogo Janja.
Aidha, anasema, kutokana na kipaji alichonacho, pia anacheza ‘serious’ filamu, ‘comedy’ na pia huimba katuni bongo fleva.
Changamoto
Pamoja na kuwepo kwa mafanikio mengi katika tasnia ya filamu na uigizaji kwa ujumla, Kitale anasema, bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wasanii, ikiwamo tabia ya wacheza filamu kuwadharau ‘macomedian’ na kuongeza kuwa, anayesababisha yote haya ni mfanyabiashara wa Kihindi, anayesambaza kazi za wasanii.
Akitoa mfano, anasema hata malipo yao yanatofautiana wanapowapelekea kazi, kwani zile za ‘comedian’ hulipa kuanzia sh 800,000 hadi milioni moja, lakini ukija kwa wacheza filamu, kazi yake moja hulipwa kuanzia sh milioni 10 hadi 12, hivyo kufanya wasanii wa vichekesho kuendelea kudharauliwa na kutokuwa na maendeleo.
“Kuna usemi usemao, kuchekesha watu ni kazi, na hivi ndivyo ilivyo jamani, kwani tunajikuta tukitumia nguvu nyingi katika kubuni kitu gani tuje nacho ili watazamaji waweze kuburudika, tofauti na wenzetu, wao wanaweza ‘wakacopy na kupaste’ hata filamu za nje, zaidi watabadilisha lugha, lakini ukija kwenye malipo ndiyo hivyo tena, wao wanalipwa zaidi,” anasema.
Mafanikio
Katika mafanikio, anasema si mabaya ukilinganisha na huko nyuma alipokuwa akiigiza tamthilia.
Japokuwa hakutaka kuwa wazi katika mafanikio aliyoyapata, anasema kwa sasa hafikirii kabisa suala la kuigiza tamthilia, labda aje mtu atakayeweza kumlipa kiasi atakachoridhika nacho.
Ushauri
Akianza na wasanii wenzake, Kitale anasema ni vema wakawa na umoja wa kweli ili kutetea haki zao, ambazo wamekuwa wakizikosa kwa muda mrefu, badala ya unafiki unaofanywa sasa hivi, ambapo baadhi ya wasanii wenye majina wamejitenga na kuanzisha ‘club’ yao.
Kwa upande wa serikali, anasema ni vema ikatambua kazi za wasanii na kutoa mfano wa nchi kama ya Marekani, wasanii wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi hiyo.
Pia ametaka haki za wasanii kuwekwa katika sheria za nchi, ili iwe rahisi kwenda katika vyombo vya sheria pale wanapofanyiwa ndivyo sivyo.
Kwa jamii, Kitale anasema, isiwe inawachukulia waigizaji kuwa wanavyoigiza ndivyo tabia zao, bali wanafanya vile ili kufikisha ujumbe.
Katika hilo anasema hata yeye anavyoigiza kama teja, hajawahi hata siku moja kuvuta bangi wala mihadarati, ila ujuzi wa kuigiza uteja ameupata kutokana na mazingira aliyokulia ya Mwananyamala Kisiwani jijini Dar es Salaam, kuwa na watu wa aina hiyo.
“Mashabiki wangu nataka muelewe kuwa mimi ni kijana safi na ninamcha Mungu, ila wanayoyaona nikiigiza ni katika kutoa mafunzo kwa vijana wenzangu, kwani dawa za kulevya si kitu kizuri,” anasema Kitale.
Musa Kitale alizaliwa mwaka 1986 akiwa ni mtoto wa kwanza miongoni mwa wanne wa familia ya Mzee Yusuph Musa na mama Mwanahawa Abdallah, akiwa na asili ya Mkoa wa Morogoro.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment