Monday 18 June 2012

CHADEMA YAVUNA VIGOGO WA CCM!!!!


NI KATIKA MIKOA YA IRINGA, SINGIDA,NAPE AWABEZA, AWAFANANISHA NA OILI CHAFU
Tumaini Msowoya, Iringa
WIMBI la viongozi na makada wa CCM kuhamia vyama vya upinzani linaendelea kukitikisa chama hicho, baada ya viongozi wa chama hicho mikoa ya Iringa na Singida kujiunga Chadema.Chadema kimewateka makada hao kilipofanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kihesa Sokoni, juzi mjini Iringa kwa lengo la kuendeleza mkakati wake wa Movement For Change-M4C (Vuguvugu la Mabadiliko) na kufafanua bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13.
Wimbi la makada wa CCM kuhamia Chadema lilipamba moto Aprili mwaka huu baada ya Ole Millya kuondoka akifutiwa na viongozi kadhaa wa chama hicho, akiwamo Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM Wilaya ya Longido, wenyeviti watano wa vitongoji na wanachama 2,402 wa CCM wilayani Ngorongoro.
Viongozi wa CCM waliojiunga Chadema jana, ni Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Iringa Vijijini, Yohana Mwena na Mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Umoja wa Vijana (UVCCM) wilayani humo.

Wengine ni Katibu wa UV-CCM Mkoa wa Singida anayesoma katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) kilichopo Iringa, Kasifia Sumpta, mwanazuoni wa chuo hicho, Dk Matabazi Lugazia, na kada wa siku nyingi wa chama hicho, Zuberi Mwachura ambaye alirejesha kadi sita za CCM kutoka katika familia yake.
Licha ya Chadema kupewa kibali cha kufanyia mkutano huo kwenye uwanja mdogo uliozungukwa na barabara zenye magari mengi, umati wa watu ulifurika, huku wengine wakilazimika kukaa juu ya nyumba na miti.
Katika mkutano huo ambao ulihutubiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM,  Mkoa wa Arusha, James ole Millya na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, wanachama wengine zaidi ya 200 wa CCM walirudisha kadi na kujiunga na Chadema.

No comments:

Post a Comment