UPANDE wa jamhuri katika kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shaaban Mintanga, umeshindwa kuleta mashahidi mahakamani hapo kwa kukosa fedha za kuwasafirisha.
Wakili wa Serikali Anselm Mwampoma, alidai gharama za kuwaleta mashahidi watano kutoka nchini Mauritius, ni dola milioni 19 za Marekani kiasi ambacho serikali imeshindwa kumudu, hivyo wanafanya uwezekano wa kupata sauti na picha zenye ushahidi.
Kabla Jaji anayeisikiliza Dk. Fauz Twahib kuiahirisha hadi Julai 16, mwaka huu, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Jerome Msemwa, walilalamikia kitendo hicho na kudai ni mpango wa serikali kuhakikisha mteja wao anafia mahabusu kwa kufanya uzembe wa kutowafuatilia mashahidi.
Wakili Msemwa alidai mahakamani hapo kuwa wakili wa serikali anapokea maagizo ya kuchelewesha kesi hiyo kutoka juu (bila kufafanua juu kwa nani) kuja kuomba muda zaidi wakati sheria ipo wazi kwamba iwapo mashahidi hawatapatikana, upande wa ushahidi unapaswa kufungwa.
“Mtuhumiwa anateseka rumande kutokana na hali yake… anaumwa moyo huku akitaabika bila sababu za msingi; ni bora mngetoa hukumu ya kifungo kuliko kumtesa. Namna hii inaonekana serikali iko juu ya mahakama,” alisema wakili Msemwa.
Akijibu hoja hizo, wakili wa serikali alipinga kupewa maagizo kutoka serikalini kwa kuwa mhimili huo uko kwa ajili ya wananchi, hivyo usingependa kuona raia wake akisota rumande na kusema, Msajili wa Mahakama Kuu ndiye aliyesema hakuna fedha za kuwasafirisha mashahidi.
Kesi hiyo iliyofunguliwa Julai 4, 2008, hadi sasa haijaanza kusikiliza mashahidi wake huku Mintanga akizidi kusota mahabusu.
No comments:
Post a Comment