MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewataka mawakili wa utetezi na wale wa jamhuri kuwasilisha uthibitisho wa umri wa msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ kabla ya kutoa uamuzi wake Juni 25, 2012.
Agizo la mahakama hiyo lilitolewa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib, anayesikiliza madai ya utata wa umri wa msanii huyo nyota wa maigizo nchini.
Kabla ya kuahirisha kwa kesi hiyo, Jaji Twaib alizitaka pande hizo mbili kupeleka vithibitisho vya hati ya kiapo cha cheti cha kuzaliwa cha Lulu kujiridhisha umri sahihi.
Kwa upande wake wakili wa mshtakiwa, Flugency Massawe, alidai mahakamani hapo kuwa hadi Juni 13 atakuwa amewasilisha huku wakili wa serikali, Elizabeth Kaganda akisema atawasilisha Juni 22.
Lulu anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba Aprili 7, mwaka huu, anadai kuwa ana umri chini ya miaka 18 huku jamhuri ikipinga kwamba ana zaidi ya umri huo.
Pamoja na Massawe, mawakili wengine wanaomtetea mshtakiwa huyo ni Jacqueline Dimelo, Kennedy Fungamtama na Maico Kibatala huku Kaganda akisaidiwa na Shadrack Kimaro kwa upande wa Serikali
No comments:
Post a Comment