Wednesday, 24 July 2013

Kwa Mbowe haramu, kwa JK halali?


MIMI nimetumwa kuuliza tu, nimeombwa na Watanzania, wazalendo wanaopenda nchi yao, kuwa huu utaratibu wa kudai ushahidi kwa nguvu unaotumiwa na jeshi la polisi umeanza kutumika lini? Na kwa nini umeanzia kwa Mbowe tu?
Wengine wengi waliowahi kusema wana ushahidi na wakautoa polisi ulitumikaje? Nimeambiwa nisisahau kuuliza, mbona Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa anao ushahidi wa wauzaji wa dawa za kulevya, na sasa taifa letu linakabiliwa na tatizo hilo, na tunasumbuka kuliondoa.
Kikwete hajawahi hata siku moja kuonyesha orodha, tatizo bado lipo, je mbona polisi hawakwenda kudai ushahidi kwa kutuma barua ya amri kama walivyofanya kwa Mbowe?
Watu hao wanasema Mbowe amegoma kuleta ushahidi, si kwamba hataki kuutoa, anataka kuutoa kwa mamlaka iliyo huru ili wanaotuhumiwa wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Kwa nini polisi wanalazimisha kuwa mahakimu kwa kesi inayowahusu? Kosa wamefanya wao, uchunguzi wafanye hao, ushahidi wapewe wao, maelezo ya kesi waandike wao, sasa wanatafuta nafasi ya kujihukumu, je haki itatendeka?

Nimeombwa kuwakumbusha polisi, kwa matukio yale ambayo ushahidi uko wazi walichukua hatua zipi kuonyesha uadilifu wao kwa Watanzania?
Akizungumza chini ya kiapo Dk. Stephen Ulimboka alimtaja ofisa wa Ikulu, Ramadhan Ighondo, kuwa ndiye aliyehusika kumteka na kumtesa, alisema vile akiwa mahututi, na akiwa mzima baada ya matibabu.
Huu ushahidi wa wazi uliotolewa polisi walichukua hatua gani? Suala la Dk. Ulimboka lilitikisa nchi, likachafua jina la nchi yetu nje na ndani, tena serikali ndio ikatajwa kuhusika, kwa nini polisi hawakuwa na uchungu wa kuchukua ushahidi huo na kuufanyia kazi kama sheria za nchi zinavyopaswa?
Siku Emmanuel Nchimbi alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya polisi, alimtaja kigogo mmoja wa jeshi la polisi kwa kashfa ya kuchangisha pesa kwa watoto wa walala hoi na kuwapeleka chuo cha polisi, huko Moshi.
Licha ya Nchimbi kusema siku hiyo wamemsimamisha kigogo huyo wakamtaja kwa jina la Renatus Chalamila, Nchimbi alisema wamemsimamisha kwa mwezi mmoja wakisubiri Rais arudi kutoka ziara nje ya nchi, mbona hatujaambiwa hatua gani zilichukulikwa kwa ushahidi uliopatikana kwa suala hilo la wazi?
Tume ya Haki na Utawala Bora, iliyochunguza sakata la kuuawa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi ilisema aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, ndiye alikiuka sheria kwa kutoa amri isivyo halali, akasababisha mauaji ya Daudi Mwangosi.
Kwa ushahidi huu wa wazi, uliotolewa hata kwa picha na watu waliokuwepo kwenye eneo la tukio, je polisi walishachukua hatua zipi kwa ushahidi huo? Kama hawajachukua ni kwa nini?
Huu sio mtazamo wangu, ila ni hofu ya wazalendo wanaoipenda nchi, wanasema kumlazimisha Mbowe atoe ushahidi unaowatuhumu ninyi kuwa ni wahusika wakuu wa kulipua bomu la Arusha kunaweza kuwa aibu ya jeshi.
Fikirini muda ambao ushahidi huo wamebaki nao viongozi wa CHADEMA, je mna uhakika anao Mbowe peke yake? Ikitokea mkamkamata Mbowe, makundi mengine yakautoa- pengine alishayakabidhi-si itakuwa aibu ya jeshi letu?
Mabomu yote yalilipuka Arusha, bomu lililolipuka kanisani hadi sasa jeshi halijasema lilitoka wapi, licha ya kumshikilia kijana mmoja kwa sakata hilo.
Kuhusu bomu hili lililolipuka kwenye mkutano wa CHADEMA, ambalo jeshi la polisi limesema kuwa lilitengenezwa China, kwa nini serikali haitaki kuiuliza serikali ya China ilimuuzia nani bomu hilo?
Na alipouziwa sheria za kimataifa zilifuatwa kama zinavyohitaji kufuatwa kwa sheria za uuzaji wa silaha kimataifa? Kama hazikufuatwa je, Tanzania iko tayari kuitaja China kuwa inafadhili vikundi vya kigaidi nchini? Kama hayo hayawezekani kwa nini ushahidi utafutwe kwa nguvu?
CHADEMA imesema inataka Rais aunde tume, Rais hajasema haundi tume, je jeshi la polisi limepata wapi ujasiri wa kuingilia mchakato wa kisheria?
Je, inaruhusiwa mchakato mmoja wa kisheria kuingilia mchakato mwingine?
Jeshi la Polisi lijipange vema kuhusu sakata la bomu la Arusha kwani njia linazotaka kuzitumia zitaiingiza nchi kwenye machafuko.
Busara zitumike, polisi subirini Rais aseme haundi tume, na mtafute ushauri mwingine wa kisheria.
Ushahidi unaotumika mahakamani na ambao mnauzingatia kulazimisha utaratibu wa jeshi kupata ushahidi unaweza kulidhalilisha jeshi.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment