Miongoni mwa wazamiaji walioshindwa kufanya kazi ya uokoaji baada ya meli ya Mv Skagit kuzama katika eneo la Chumbe na Dar es Salaam wiki iliyopita ni Muhsin Salum Muddy .
Mzamiaji huyo anasema baada ya kupinduka meli hiyo alipoteza fahamu wakati wa zoezi la kuwaokoa watu waliopata ajali hiyo.
“Sikujitambua mie, na sijui nimefikaje hospitalini hapa maana nafungua macho ndio najiona nipo katika kitanda na nimefunikwa blanketi, ninachokijua mie ni kwamba niliingia katika boti ya polisi kwenda kuwaokoa watu waliopata ajali” alisimulia kijana huyo na kuongeza:
“Pamoja na kwenda kuwaokoa walionusurika katika boti na kuchukua maiti nilikuwa na kamera kwa ajili ya kupiga picha lakini nikashindwa kufanya kazi zote kutokana na hali ya hewa ilivyokuwa mbaya” alisema.
Kushindwa kufanya kazi kwa Muddy kulitokana na mawimbi makali baharini ambayo yalisababisha boti za uokoaji kushindwa kutulia kufanya kazi hiyo, ambapo waokoaji wengine walikumbwa na mkasa kama wa kwake na wengine kujeruhiwa vibaya.
“Tuliondoka Bandari ya Malindi saa 9:30 jioni na tukafika kule saa 12 na baada ya nusu saa ndio tukawa tunaziona maiti zikielea na watu waliokuwa hai wakiomba msaada wa kuokolewa huku wakihangaika sana na kuonyesha kuchoka, wengine tayari walishakunywa maji mengi na kuhitaji msaada lakini haikuwa rahisi kufanya kazi hiyo” alisema.
Kutokana na hali ya bahari kuchafuka sana, baadhi ya vyombo vililazimika kurudi bila kufanya uokoaji, ambapo Muddy alisema wenzake wengi waliokuwa ndani ya boti walitapika sana na kuishiwa nguvu.
Akisimulia tukio lililomkuta kijana anayekadiriwa kuwa na miaka 30, alisema wakati wakikaribia kufika eneo la ajali chombo walichokuwa wamepanda kilipigwa na mawimbi makali na yeye kupatwa na kichefuchefu na hatimaye kutapika na kuishiwa nguvu kabisa.
Alisema wakati yeye akiwa taabani aliwaona wazamiaji wenzake wakitapika sana huku maiti na miili ya watu wanaotaka kusaidiwa wakiwa wanaonekana karibu na boti za uokoaji zilizojitokeza kufanya kazi hiyo huku baadhi ya maiti zikizagaa baharini.
Endelea kusoma hapa:http://www.mwananchi.co.tz/habari/-/24979-mzamiaji-aibua-mapya-ajali-ya-mv-skagit
No comments:
Post a Comment