Friday, 10 August 2012
AJALI ZITAENDELEA KUANGAMIZA NGUVU KAZI YA TAIFA MPAKA LINI?
KWA mara nyingine Watanzania wameingia katika majonzi kufuatia ndugu zao zaidi ya 17 kufa na wengine 78 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora Jumanne iliyopita.
Taarifa ambazo ziliripotiwa na vyombo vya habari jana zimeonyesha kuwa, basi hili lililotoka Tabora kuelekea mkoani Mbeya lilipinduka kwenye kona wakati dereva analikwepa lori lililokuwa linakuja mbele yake.
Ni jambo la kusikitisha kuwa, ajali za barabarani zinaendelea kuua Watanzania kila kukicha bila mamlaka zinazohusika kuchukua hatua zinazostahili kukabiliana na mazingira ya kizembe yanayosababisha maafa hayo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali za ajali hiyo, ni dhahiri dereva wa basi hilo alikuwa na makosa ya kuendesha mwendo kasi ndiyo maana alipoona lori mbele yake alishindwa kulidhibiti na kusababisha gurudumu kupasuka kisha gari kupinduka na kuua watu wengi kiasi hicho.
Pili, basi hilo lilikuwa na makosa ya kubeba abiria wengi kinyume cha sheria. Taarifa zinasema kuwa watu 17 walikufa na wengine 78 wamejeruhiwa, ikimaanisha kuwa lilikuwa na abiria wanaokaribia 100, kwani bila kutoa idadi ya walionusurika, hesabu ya vifo na majeruhi inafikia watu 95. Ni basi gani linalobeba abiria zaidi ya 95!
Sote tunafahamu kuwa asilimia kubwa ya mabasi yanayofanya safari ndefu yanabeba abiria kati ya 55 na 65, sasa hao 30 waliozidi katika basi hilo walikaa wapi na vyombo vya dola vilikuwa wapi mpaka likajaza zaidi ya uwezo wake?
Na jambo la kushangaza miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo alikuwamo askari ambaye imeelezwa kuwa alilalamika kwa askari awa Usalama Barabarani, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Ni kwa nini hawakuchukua hatua? Hili ni swali linalotoa picha nyingi za jinsi uwajibikaji wa Watanzania katika kudhibiti uhalifu ulivyooza.
Ukifuatilia ajali nyingi zinazotokea nchini, iwe kwa mabasi na vyombo vya usafiri wa majini; taarifa zinaonyesha kuwa huchangiwa na kuzidisha abiria. Kwa mfano, ajali za mabasi karibu zote huonyesha kuwa pamoja na mwendo kasi, abiria wanakuwa wengi zaidi ya uwezo wake.
Pili, karibu taarifa zote za ajali mbaya za meli, ukianzia Mv Bukoba katika Ziwa Victoria, Mv Islander na Mv Skagit katika Bahari ya Hindi huonyesha kuwa zilizidisha idadi ya abiria kwa kiwango kikubwa, ukiachia ubovu na matatizo mengine ya kiufundi ya vyombo hivyo.
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba, mamlaka na vyombo vinavyohusika hufuatilia kwa karibu ajali zinapotokea, lakini baada ya muda mfupi hunyamaza na kuacha wamiliki na waendesha vyombo hivyo wafanye mambo wanayotaka kinyume cha sheria. Tunamaanisha kuwa, kwa jumla uwajibikaji mbovu ni tatizo kubwa hapa nchini.
Sisi tunajiuliza kwamba, tatizo liko wapi wakati sheria zipo? Kwa nini vyombo na mamlaka zinazohusika zinashindwa kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati kuhakikisha kuwa ajali zinazomaliza nguvu kazi ya taifa zinakomeshwa, kwa kuzisimamia kikamilifu sheria? Kama sheria zilizopo hazifanyi kazi zifutwe na kutungwa zenye makali yanayokata pande zote.
Tatizo la kujaza abiria ni sugu si tu katika mabasi yanayokwenda mikoani, bali hata mabasi yanayotoa huduma za usafiri mijini. Kwa mfano, utakuta basi linalotakiwa kubeba abiria 25 linabeba mpaka 50! Watu wakilalamika kondakta na dereva wanasema, “Nani kakwambia daladala inajaa, sogea huko, vinginevyo shuka kapande teksi.” Na wakati huo tayari ameishatoza nauli!
Katika Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi pekee iliyoacha mabasi kujaza abiria kupita kiasi, kwani nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda zimefanikiwa kudhibiti tatizo hilo kwa kusimamia sheria zinazotaka abiria katika mabasi yote (hata daladala) wakae kwenye viti akiwamo kondakta wake. Madereva wanatii kwa kuwa polisi na vyombo vyote vya usimamizi wa sheria vinafanya kazi ipasavyo.
Hivi kweli sheria zetu hazina makali na wala wasimamizi wake hawana meno, au mfumo wa rushwa umedhoofisha kabisa makali ya sheria na uwajibikaji!
Kwa jumla, hali inapofikia katika hatua hii ni hatari kwa ustawi wa taifa letu, kwani ni kama watu wameachwa wafanye wanavyotaka kwa kuwa wana nguvu ya pesa.
Tunawashauri viongozi wa Serikali na mamlaka zake wabadilike na utawala wa sheria lazima uchukue mkondo wake kwa nguvu zote kunusuru maisha ya Watanzania na ustawi wa taifa letu.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment