Hatimaye askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, amefikishwa mahakamani kwa shitaka la mauaji.
Askari huyo mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simon (23), mkazi wa FFU Manispaa ya Iringa, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi ya Wilaya jana akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Mwangosi.
Mashtaka hayo alisomewa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Michael Luena.
Luena alidai mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Dyness Lyimo, kuwa Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, mtuhumiwa huyo alimuua Mwangosi, kinyume cha kifungu cha sheria namba 148 (5A) (i) cha makosa ya jinai.
Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji kisheria.
Mtuhumiwa alirudishwa mahabusi kutokana na kesi yake kutokuwa na dhamana kisheria.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 26, mwaka huu, itakapotajwa mahakamani hapo.
POLISI WAZUIA WAANDISHI KUMPIGA PICHA
Askari saba waliompeleka mtuhumiwa huyo mahakamani waliovalia kiraia, waliweka ulinzi mkali na kuhakikisha mtuhumiwa hapigwi picha.
Kutokana na hali hiyo, waandishi wa habari walipata wakati mgumu kumpiga picha mtuhumiwa huyo.
Kila walipojaribu kutaka kufanya hivyo, walijikuta wakisukumwa na askari hao kuzuiwa wasimpige picha mtuhumiwa huyo.
Mtuhumiwa huyo alipelekwa kwa mwendo wa haraka kwenye gari lenye namba za usajili T320 ARC aina ya Toyota Land Cruiser GX tofauti na kawaida ya gari linalotumiwa na mahabusu pindi wanapofikishwa mahakamani.
Kadhalika mtuhumiwa huyo alifunikwa kitambaa sehemu za kichwani na kuvalia koti la rangi nyeusi, kiasi cha kumfanya ashindwa kutembea vema.
Hali hiyo ilisababisha kiatu chake kimoja aina ya sandozi kukatika na kubaki katika eneo la viwanja vya mahakama hiyo baada ya gari lililombeba kuondoka eneo hilo.
Mwangosi aliuawa akiwa kazini baada ya kupigwa na bomu lililosambaratisha sehemu kubwa ya mwili wake.
Alikumbwa na mkasa huo wakati polisi wakiwatawanya viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ILI kuwazuia wasifungue tawi la chama hicho katika Kata ya Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Mauaji ya mwandishi huyo yalilaaniwa vikali na makundi kadhaa ya jamii, ambao walitaka uchunguzi huru ufanyike kubainisha hasa chanzo cha kadhia hiyo.
Miongoni mwa wadau waliojitokeza kupinga na kulaani kwa nguvu zote mauaji hayo, ni Chadema.
Chadema kilipendekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, IGP Mwema, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Kamishna Paul Chagonja, wawajibike kwa kujiuzulu nafasi zao, kutokana na mauaji ya raia katika mikoa ya Morogoro na Iringa kutokea mikononi mwa jeshi hilo, ambalo lipo chini ya usimamizi wao.
Walisema iwapo viongozi hao watashindwa kuwajibika, basi Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi.
Pia walitaka Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Michael Kamuhanda, pamoja na Mkuu wa FFU mkoani humo, wawajibike kwa kujiuzulu kwa sababu hiyo.
Wakati sauti hizo zikipazwa, waandhishi wa habari karibu nchini kote, juzi na jana walifanya maandamano ya kimya kimya kulaani mauaji ya mwenzao.
Pamoja na mambo mengine, waandishi walilitaka jeshi hilo lirejeshe vitendea kazi vilivyokuwa vikimilikiwa na Mwangosi, ikiwamo kamera, kompyuta (laptop) pamoja na simu ya mkononi, alivyokuwa navyo wakati akiwa mikononi mwa askari polisi zaidi ya wanane kabla ya kuuawa.
Kadhalika, Mkuu wa Jeshi Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, pamoja na maofisa wengine waandamizi wa jeshi hilo, walikutana na viongozi wa Chadema na kuzungumzia hali ya baadaye baada ya kutokea kwa mauaji hayo.
Vilevile, Waziri Nchimbi aliunda kamati inayoongozwa na Jaji Stephen Ihema ili kumsaidia pia kupata majibu ya maswali, ambayo hana majibu yake kuhusiana na kifo hicho.
chanzo:nipashe

No comments:
Post a Comment