Saturday 27 October 2012

DIAMOND ADAI HANA MPANGO WA KUOA SASA!


MWANAMUZIKI wa muziki wa Bongo fleva, Naseeb Abdul, ‘Diamond’ amesema hana mpango wa kuoa siku za karibuni kwa kuwa bado anahitaji sana mapenzi ya karibu na mama yake.
Akihojiwa katika kipindi cha ‘Mcheza Kwao’, Diamond alisema kumekuwa na maneno mengi yaliyozagaa kuwa hivi karibuni atamuanika mchumba wake anayetaka kufunga naye ndoa, jambo ambalo si la kweli.
Diamond, ambaye unaweza kusema ndiye mwanamuziki anayefunika kwa sasa katika miondoko ya Bongo fleva, kutokana na nyimbo zake kupendwa na watu wengi, alisema mbali na kuhitaji mapenzi kwa mama yake, pia ushauri wake ni jambo la muhimu katika kila jambo analotaka kulifanya.
“Unajua mimi ninampenda sana mama yangu na ndiye kila kitu kwangu, hivyo najikuta hakuna kitu ninachoweza kufanya bila kumjulisha, hivyo kuwa naye mbali kwa sasa itakuwa ngumu,” alisema.
Akizungumzia kuhusu uhusiano wake na aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, alisema kwa sasa ni rafiki yake wa kawaida, si mpenzi na wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali.
Kwa mujibu wa Diamond, matatizo yote yaliyotokea huko nyuma, wameshasameheana na sasa hivi wanaiva vilivyo.
Diamond na Wema walishawahi kuwa wapenzi na kujikuta wakimwagana mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo habari zao ziliteka vyombo mbalimbali vya habari, hasa pale mwanamuziki huyo alipofanya onesho lake Mlimani City na kuzikataa fedha alizotuzwa na mwanadada huyo.
Kama vile haitoshi, walikuwa wakirushiana vijembe kila mmoja akimtuhumnu mwenzie kuwa hajatulia.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment