Monday 15 October 2012

UTATA WAGUBIKA KIFO CHA RPC BARLOW!!!!



Utata umegubika mauaji ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa Barlow, aliuawa maeneo ya Kitangiri katika barabara inayoelekea Bwiru, jirani na hoteli ya Tai Five jijini hapa. Alisema mauaji hayo yalifanyika kati ya saa 7 na saa 8 usiku, wakati Barlow akimsindikiza mwanamke aliyejulikana kama Doroth Moses. Inasemekana kuwa wote wawili, walikuwa wametoka kuhudhuria kikao cha maandalizi ya harusi ya mtoto wa dada wa Barlow, kilichofanyika hoteli ya Florida.
Hata hivyo, taarifa zisizo rasmi kutoka mitandao ya kijamii kuhusu utata wa mauaji hayo, zinaeleza kuwa Barlow na mwanamke huyo walikuwa wanatoka katika hoteli inayotajwa kwa jina la La-Kairo. Akifafanua, Ndikilo alisema Barlow alikuwa akiendesha gari yake binafsi aina ya Toyota Hilux- double cabin na kwamba alikuwa akimsindikiza mwanamke huyo kwenda nyumbani kwake.
Mwanamke huyo ambaye anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi, ni mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamagana. Alisema wakati wakikaribia eneo la Kitangiri anakoishi mwanamke huyo, waliwaona watu wawili wakiwa wamevaa mavazi maalum (jackets) yanayovaliwa na wananchi wanaoshiriki ulinzi shirikishi unaofahamika pia kama polisi jamii. Kwa mujibu wa Ndikilo, baada ya kuwaona watu hao ambao waliwamulika kwa tochi, Doroth alimuuliza Barlow iwapo anawafahamu, naye alimjibu kuwa watakuwa ni polisi jamii.
Hata hivyo, Ndikilo alisema baada ya Barlow kusimamisha gari pembeni, mkabala na nyumba anayoishi mwanamke huyo, watu hao wawili waliwasogelea huku wakionyesha kukerwa na mwanga wa taa za gari. Alisema watu hao walimhoji Barlow kwa nini anawamulika kwa taa za gari, lakini wakati akijaribu kutoa ufafanuzi kwamba yeye ni RPC, ghafla walitokea watu wengine wapatao watatu, walisimama kuzunguka gari la Kamanda huyo.
Baada ya kuona hali hiyo, huku akijaribu kuwauliza iwapo hawamfahamu kuwa yeye ndiye RPC na kutoa radio call (simu ya upepo) ili kufanya mawasiliano na polisi wa doria. “Ghafla mmoja wa watu hao alitoa bastola na kumfyatulia risasi ambayo iliingilia shingoni na kutokea upande wa pili wa bega,” alisema Ndikilo.
Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walichukua vitu kadhaa ikiwemo bastola, simu na radio call alivyokuwa navyo Barlow na kutoweka kusikojulikana. “Kimsingi mazingira ya mauaji yenyewe bado yana utata, lakini Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tunafanya kazi ya kuchunguza ili kuujua ukweli,”alisema.
Kwa mujibu wa Ndikilo, baada ya kufyatuliwa risasi inaaminika Barlow alikufa papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando ukisubiri taratibu za mazishi. Alisema kutokana na mazingira hayo ya utata ya mauaji, Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamke aliyekuwa naye kwa mahoajiano zaidi. Taarifa za awali zilidai kwamba mwanamke huyo anayesadikiwa kuwa ni mjane, ni dada yake Barlow.
Lakini baadaye jana, Mkuu wa mkoa wa Mwanza alikanusha taarifa hizo na kusisitiza kuwa ni mtu ambaye alikuwa amempa lifti wakati wakitoka katika kikao cha harusi. Kufuatia mauaji hayo Ndikilo alisema kuwa Polisi Makao Makuu, limemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio hilo.
Nyumbani kwa Doroth, kijana Kenrogers Edwin aliyejitambulisha kama mtoto wa kaka yake wa mwanamke huyo, alisema kabla ya tukio hilo, shangazi yake (Doroth) alipiga simu ili wamfungulie geti. Alisema kwamba wakati akifungua geti, aliona gari likiwa limeegesha huku watu wawili wakiwa upande wa abiria na wengine watatu wakiwa upande wa dereva na kisha alisikia mlio wa risasi na baadaye watu hao walitimua mbio baada ya kuona pikipiki inakuja nyuma yao.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia mauaji hayo walielezea kushangazwa kwao na hatua ya Barlow kutembea usiku bila mlinzi wake (bodyguard) ambaye kwa kiwango kikubwa angeweza kusaidia kumuepusha na kifo.
Chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment