Friday, 23 November 2012

Nchimbi ang`aka mfungwa kutolewa gerezani kinyemela


Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema ni kitu ambacho hakiwezekani kwa mtu ambaye anatumikia kifungo gerezani atolewe kienyeji na kupatikana na silaha uraiani.
Akizungumza na NIPASHE jana kuhusiana na utata wa sakata la mfungwa aliyekutwa uraiani akiwana bunduki na risasi, alisema Jeshi la Magereza ndilo lenye mamlaka ya kuelezea taarifa kwa usahihi kuhusu mfungwa aliyoko gerezani.
“Hili jambo vyombo vya habari vinataka kulikuza tu, kimsingi wenye mamlaka ya kueleza taarifa za mfungwa ni Magereza na siyo polisi,” alisema Dk. Nchimbi.
Dk. Nchimbi ambaye hata hivyo hakutaka kuelezea kwa undani sakata hilo, alisema kwa taratibu za kijeshi kauli inayosimama ni ya Kaimu Kamishna wa Magereza, Deonice Chamulesile.
Alisema Chamulesile ametoa ufafanuzi ambao unaoeleweka kwamba Masanja Maguzu (42) alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano, lakini Aprili 26, mwaka huu aliachiwa huru.
“Mfungwa aliyekuwa na Namba 250/2010, Masanja Maguzu, alipokelewa Gereza la Wilaya ya Shinyanga tarehe 3 Novemba, 2010 baada ya kuhukumiwa na Mahakama ya wilaya hiyo kwa makosa mbalimbali ya uhujumu uchumi,” alisema.
Aliongeza: “Alianza kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kuanzia Novemba 3, 2010 na kufikia Aprili 26, 2012 aliachiliwa baada ya kutimiza masharti ya kifungo na kutoka gerezani kwa mujibu wa sheria, hivyo ifahamike kwamba hakutoka katika mazingira ya utata kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari.”
Taarifa hiyo iliyataja makosa aliyohukumiwa kuwa ni kuingia kinyume cha sheria katika hifadhi, kuwinda kunyume cha sheria na kumiliki kinyume cha sheria nyara za serikali.
Waziri Dk.Nchimbi alisema kutokana na ufafanuzi wa Chamulesile, hivyo wananchi wafahamu kuwa mtu huyo alikuwa amemaliza kifungo hivyo hakuna utata wowote katika jambo hilo.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Simiyu lilieleza kuwa Msanja Maguzi aliyekamatwa nyumbani kwake Novemba 16, mwaka huu akiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), risasi 31 na magazini tatu, ni mfungwa ambaye hajamaliza kutumikia kifungo cha miaka 15 jela na kuwa alitoka gerezani katika mazingira ya kutatanisha.
Baadaye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alisisitiza kuwa Maguzu alikuwa hajamaliza kifungo hicho jambo ambalo limeleta mkanganyiko kwa jamii ambayo inashindwa kuelewa mkweli ni nani.
Hata hivyo, jana, Kamanda huyo akisema suala hilo ameliachia mamlaka nyingine.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment