Friday, 30 November 2012

Simu kukebehi wafu siyo uungwana


MZAHA mzaha umekuwa ukiongezeka miongoni mwa jamii kila linapotokea tatizo, liwe kama ni janga au hata furaha baadhi ya watu hutumia mzaha huo.
Baadhi ya watu hao wamekuwa wakikosa maadili na kupoteza mshikamano katika matukio mbalimbali mbayo yanahitaji kusaidiana na kuwafariji wahusika.
Kikubwa anbacho nitakizungumzia leo ni kuhusu matumizi mabaya mtandao hasa simu; kwa kweli ni aibu kwa taifa ambalo linaaminika kuwa la watu wenye umoja na mshikamano.
Matumizi hayo mabaya ya simu yamekuwa yakitumika katika kudhihaki matukio kama vile misiba ikiwemo ile ya watu maarufu nchini.
Ustaarabu wa Watanzania umekuwa ukishuka kutokana na kuyachukulia matukio hayo ya vifo kama mambo ya kufurahisha katika jamii.
Kifo cha Msanii Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Millionea’ chahusika: kuna baadhi ya watu ambao hawana utu wa kibinadamu; wamekuwa wakikichukulia kwa mzaha kwa kutumiana ujumbe ambao hauna maana yoyote sanasana kuwaongezea huzuni wafiwa.
Ukiangalia ujumbe unaotumwa na watumiaji simu hao hata haueleweki una lengo gani na ni kwa faida ya nani haswa.
Ujumbe wa kumkebehi mtu ambaye amekwishafariki kwa kweli unasikitisha sana; hivi ni vitendo ambavyo havistahili kuungwa mkono na kila mmoja ambaye anajua maana halisi ya kufiwa.
Kwa mfano ukiangalia ujumbe unaosema, “Sharo: Mnanizika wapi meeen? Majuto: Muheza Tanga; Sharo : Mmebugi meen nataka mnizike alipozikwa Michael Jackson meeen! Majuto: We unazikwa Lusanga kijijini. Sharo: Ooh mamaaaa!
“Kanumba: Kwani vipi mbona una mawazo na tayari umeishafika kwenye makazi ya milele! Sharo: Haya mawazo nawaza jee mazishi yatafanana kama na ya kwako yalivyokuwa meeen?
“Kanumba: Karibu sana Sharomilionea huku ndiko Airtel ulikokuwa unataka kuhamia, bado mzee wako Majuto!”
Huo ni mmoja wa ujumbe ambao umekuwa ukisambazwa na watu ambao unaweza kuwaita kuwa ni watu wenye mtindio wa ubongo na waliochanganyikiwa na maisha huku wakikosa kazi za kufanya.
Ujumbe kama huo uko wa aina nyingi na waandaaji wa ujumbe kama huo wamekuwa na kazi kubwa ya kuuandaa kwa malengo ya kufurahisha nafsi zao wakati wafiwa wakiteseka kwa uchungu wa kumpoteza ndugu yao.
Ukiachilia mbali hao wanaotuma ujumbe pia wapo wanaosambaza baadhi ya picha za msanii huyo ambazo kimaadili na utamaduni wa Kitanzania hazingepaswa kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa kweli huu ni udhalilishaji pia haipendezi, sijui inatufundisha nini kama siyo kuudhalilisha mwili wa marehenu ambaye hastahili kufanyiwa hivyo.
Sitaki kuamini sana kama kweli kampuni za simu zina vitengo vinavyoaandaa ujumbe kama huo na kama kweli vitengo hivyo vipo na vinatumika kwa staili hiyo basi naamini ubunifu wao utakuwa umefikia kikomo na hawawezi kuendelea.
Itakuwa ni kampuni gani hizo zisizojali matatizo ya wateja wake, bali kujali fedha hata kama wengine wanaathirika na ujumbe kama huo?
Safu hii inawatahadharisha watu wanaoandaa ujumbe kama huo kutambua kuwa iko siku nao watakufa na nafsi zao zitasutwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kikubwa Watanzania tujaribu kujiepusha na tabia ambazo haziwezi kutoa elimu ya aina yoyote katika jamii, ambayo ina mahitaji mengi katika kujiendeleza.
Mwisho wale wote waliotumiwa ujumbe wa aina yoyote na kuusambaza kwa wengine wanapaswa kutambua kuwa haukuisaidia familia ya marehemu bali wamechangia mitandao ya simu kwa ajili ya kuendeleza maslahi yao, na wao ni bure kabisa.
Hebu muulize anayekutumia ujumbe kama huo amelipwa shilingi ngapi na huo mtandao uliotumika kutuma ujumbe huo. Pia hii mitandao kama inajihusisha au haihusiki basi itoe tamko kuufahamisha umma kuwa inakuwaje vitu kama hivyo vinapitishwa kimzahamzaha katika mitandao yao huku wakiwa wanapepesa pesa macho tu?
chanzo: daima

No comments:

Post a Comment