Saturday 15 December 2012

Jela miaka 30 kwa kulawiti mwanafunzi


GODFREY Adamu (26) mkazi wa kijiji cha Saragana, amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kulipa sh laki 5 baada ya kumaliza adhabu hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia ya kumuingilia kinyume cha maumbile msichana mmoja ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Nyambono mwenye umri wa miaka 12.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Jonas Kaijage, aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 11, mwaka huu, majira ya saa 11:00 jioni, katika eneo la kijiji cha Saragana.
Kaijage alisema kuwa siku ya tukio mshtakiwa huyo alikunywa pombe ya kienyeji aina ya wanzuki yenye thamani ya sh 13,000,  mali ya mzazi wa mwanafunzi huyo na kudai kuwa fedha amezisahau nyumbani kwake, hivyo kuomba kuongozana na binti huyo ili akampatie fedha.
Alisema kuwa wakiwa njiani mshtakiwa huyo alimvutia vichakani mwanafunzi huyo na kisha akamuingilia kinyume cha maumbile yake.
Aidha ilidaiwa kuwa baada ya kumfanyia unyama huo mshtakiwa alimlazimisha mwanafunzi huyo ili wakaoge mtoni, kwa ajili ya kupoteza ushahidi na wakiwa njiani mwafunzi huyo alikimbia na kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wake, na ndipo mshtakiwa akakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Kabla ya hukumu kutolewa mwendesha mashtaka huyo aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwani kitendo alichomfanyia binti huyo ni cha kinyama.
Kufuatia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo, Richard Maganga, alimhuku mshtakiwa huyo kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na baada ya kumaliza adhabu yake amlipe fidia mwanafunzi huyo kiasi cha sh laki 5.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment