Saturday 15 December 2012

Albino arejeshewa vidole vyake


MTOTO Adam Robert (13) mwenye ulemavu wa ngozi (albino) jana alirejea nchini akitokea Canada alikokuwa akipatiwa matibabu ya viungo vilivyokatwa na watu kutokana na imani za kishirikina.
Mtoto huyo ambaye alifanyiwa unyama huo mwaka jana akiwa nyumbani kwa wazazi wake yaani baba mzazi na mama wa kambo, aliweza kusaidiwa na Shirika la Under the Same Sun linalohudumia watu wenye ulemavu wa ngozi nchini hadi kupata nafuu na kurejea nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Robert alisema mara baada ya kupatiwa matibabu kwa sasa anajisikia vizuri na kwamba anaweza kuendelea na shule.
Robert ambaye alikatwa vidole viwili na nusu vya mkono, kidole gumba na shahada huku cha kati kikiwa kimekatwa nusu, alishindwa kuendelea na shule kutokana na kukosa uwezo wa kuandika kwa kuwa alishindwa hata kushika kalamu.
Kwa mujibu wa Dk. Patrick Burugo, aliyekuwa akimpa matibabu Geita na hatimaye kwenda naye nchini Canada kwa msaada wa shirika la Under the Same sun, alisema matibabu yake yalikuwa makubwa na ya hali ya juu, ambapo ilimlazimu kutolewa kidole gumba cha mguuni na kuwekwa mkononi.
Alisema kuwa Robert alilazwa katika hospital ya Voncouver ambako upasuaji wake ulidumu kwa zaidi ya saa 13 ambapo kuna wakati madaktari bingwa wa upasuaji walilazimika hata kutoa misuli sehemu nyingine ya mwili na kuunga katika kidole hicho ili mradi kiweze kupata mawasiliano na kiweze kufanya kazi kwa haraka.
“Tumefanya upasuaji kwa zaidi ya saa 13 ambapo ilibidi kidole gumba cha mguu kitolewe na kiwekwe katika mkono na kipande cha nyama kukatwa kwenye paja na kuungwa mkononi, kwa kweli matibabu yalikuwa ni ya hali ya juu sana,” alisema Dk. Burugo.
Hata hivyo, mtoto huyo alitoa ushuhuda wake ambapo alisema hataki kurudi tena nyumbani kwa wazazi wake hao akihofia maisha yake kuwa hatarini.
Alielezea tukio zima akieleza kuwa akiwa nyumbani kwao alikuja mgeni ambaye alikaribishwa na mama wa kambo pamoja na baba yake mzazi ambapo walimtuma kama mara mbili ndani kuchukua chumvi na moto.
Wakati wakiwa wanamtuma aliweza kufanya kazi zote hizo lakini baada ya kufika muda wa kulala walimwita atoke nje na ndipo yule mgeni asiyemjua jina alipoanza kumkata vidole na sehemu mbalimbali za mwili.
Alisema wakati akiwa anafanyiwa vitendo hivyo, baba na mama yake walikuwa pembeni lakini yeye katika kujihami aliamua kumng’ata mtu huyo sehemu zake za siri na ndipo akamuachia.
“Nilimng’ata sehemu za siri akaniachia mara moja na ndipo baba akampigia simu baba mkubwa akaja nikapelekwa hospitali kwa kweli nilipata maumivu sana,” alisema Robert.

Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo, Vicky Mtekema, alisema ni furaha kubwa kwa mtoto Robert kurudi mzima huku akiwataka Watanzania kuacha kufanya vitendo hivyo vya kinyama kwa watu hao.
Naye rais na mwanzilishi wa shirika hilo, Peter Ash, aliitaka jamii ya Tanzania kuungana pamoja ili kupinga ukatili huo ambao unatokana na imani za kishirikina kwa kisingizio kwamba wanaweza wakapata utajiri.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment