Friday 7 December 2012

Mwandishi afichua unyama wa polisi


SIKU moja baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Charles Kenyela, kutoa taarifa ya kumkingia kifua askari wake anayetuhumiwa kumjeruhi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu, mwanahabari huyo amefichua ukweli wa tukio zima.
Matutu ambaye aliruhusiwa jana mchana kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya kutolewa risasi hiyo mwilini juzi, alisema kuwa unyama waliouonyesha polisi dhidi yake, kama asingekuwa mwandishi basi huenda wangemfanyia kitu kibaya kupoteza ushahidi.
Akizungumza jana muda mfupi baada ya kuruhusiwa, Matutu alifichua kuwa taarifa aliyoitoa Kamanda Kenyella juzi kwa vyombo vya habari kuhusu tukio hilo ni wazi imechakachuliwa, huku akionyesha hofu kwa raia wasiokuwa na ndugu wa kufuatilia matukio ya jamaa zao haki zao zinakuwaje.
Katika taarifa hiyo iliyowashangaza wananchi wengi wakiwemo majirani zake Matutu walioshuhudia tukio hilo, Kenyela alisema kuwa katika kuendeleza msako wa wahalifu, Desemba 4, mwaka huu, majira ya saa 3:30 huko Kunduchi Machimbo askari polisi namba F.8991 D/C Idrisa alijeruhiwa kwa panga kwenye mkono.
Kwa mujibu wa Kenyella, askari huyo aliyejeruhiwa mkono wa kulia alikuwa katika jitihada za kuwakamata watu waliokuwa kwenye nyumba ambao walihifadhiwa wakituhumiwa kuwa majambazi.
“Askari huyo akiwa na wenzake wanne baada ya kujeruhiwa alirukiwa na huyo aliyemkata panga (Matutu) na katika purukushani hizo risasi moja ilifyatuka kutoka kwenye silaha hiyo aina ya bastola aliyokuwanayo askari na kumjeruhi kwenye bega la kushoto mtu aliyekuwa akipambana naye,” alisema.
Ndipo ilifahamika baadaye kuwa mtu aliyekuwa anapambana na askari ni Shaban Matutu (30), mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima.
Kenyella aliongeza kuwa wote wawili mwandishi na askari walikimbizwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu ingawa baadaye Matutu alipelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
“Katika tukio hilo, askari wetu walifika kwenye nyumba hiyo kufuatia taarifa kutoka kwa msiri kuwa katika nyumba ya mama J iliyokuwa Kunduchi Machimbo kuna majambazi hatari. Ndipo Matutu alijitokeza na kumjeruhi askari kwa panga na hatimaye naye pia akajeruhiwa kwa risasi,” alisema.
Taarifa hiyo ya Kenyella ilionekama kumshtua Matutu ambaye alilazimika kutoa ufafanuzi upya wa kile kilichotokea siku hiyo.
Akiwa ameshika ganda la risasi aliyofyatuliwa, Matutu alidai kuwa alisikia mtu akigonga mlango na kumuita mkewe Mama J, wakati akimshauri akafungue mlango alisikia tena sauti ya kiume ya mtu wa pili na hivyo kutilia shaka watu hao.
“Nilichukua silaha ya jadi (panga) ili kujihami maana watu hao walikuwa hawajajitambulisha, na nilimwamuru mke wangu akae upande wake nami wangu kisha tukafungua mlango kidogo kuchungulia; baada ya kuona kundi la watu, tukawa tunausukuma mlango kuufunga tena.
“Wakati tunajitahidi kuufunga, askari mmoja aliruka na kuupiga teke kisha tukaanguka na mke wangu na tulipojaribu kuinuka askari mmoja alinipiga risasi ya bega,” alisema.
“Sikujua kama ni mimi ndiye niliyepigwa risasi maana nilidhani ni mke wangu ndiye kauawa lakini wakati nageuka nikaona damu zimetapakaa kwenye shati langu, ndipo nikabaini kuwa aliyejeruhiwa ni mimi,” alisema.
Alisema kuwa alipandisha hasira na kuwahoji askari sababu ya kunipiga risasi ndipo walijitambulisha kuwa wao ni askari na wanamsaka mtuhumiwa Mama J.
“Nilimuuliza yule aliye nijeruhi kama mtuhumiwa ni yule mke wangu aliyekuwa pale, akasema siye na hivyo nikarudia kumhoji ni kwa nini wakanitendea hivyo. Ghafla walijidai kuanza kunihudumia nilipowalazimisha wanipeleke hospitali,” alisema.
Ilifikia wakati askari huyo aliyemjeruhi kumlazimisha kuitoa risasi hiyo mwilini kwa nguvu kwa njia ya kumbinya lakini alikataa uamuzi huo akiona wanaweza kumuua.
“Tulikwenda kituo cha polisi Kunduchi Mtongani na kupewa fomu ya matibabu (PF3) lakini niligoma kutolewa risasi pale na wakati wanazozana wapi wanipeleke kuandika maelezo niliwaambia nimechoka wanipeleke hospitali,” alisema.
Matutu anafichua kuwa salama yake ilikuja pale askari hao wakati wanazozana, mmoja alimhoji mkewe akitaka kujua mumewe anafanya kazi gani.
“Mama J aliwaambia ni mwandishi wa habari, wakauliza wa chombo gani, akawajibu gazeti la Tanzania Daima, ndipo wakataharuki wakisema: “Toba tumekwisha, itaandikwa hiyo!”
Matutu aliongeza kuwa baada ya majibu hayo walihamasishana waachane na mpango wa
kwenda kituo kingine kugonga muhuri fomu na badala yake walimpeleka Mwanyamala.
“Tukiwa Mwananyamala baada ya madaktari kuniangalia na kunipa rufaa ya kwenda Muhimbili, nilijiwa na hofu baada ya kuona askari aliyenipiga risasi akiwa amefunga mkono wake kwa bandeji, nikataka nione kovu lake.
Matutu anasema katika hatua ya kushangaza, askari yule alifungua mkono wake na hakuwa na jeraha la panga bali mchubuko kidogo na hivyo hata daktari aliyekuwa akimhudumia aligoma kumtibu askari huyo akisema hajaumizwa chochote.
“Tukiwa pale huku maaskari wakiwazuia baadhi ya wafanyakazi wenzangu waliofika kuniona wasipige picha, askari walijaribu kila mbinu kunishawishi nisifungue malalamiko dhidi yao na ndipo manesi waliokuwa eneo hilo waliniambia nina bahati kwa vile nimeletwa nikiwa hai.
“Hapa tunaletewa watu wakiwa hoi au wamekufa na wanatupwa hapa kisha askari wanaondoka halafu kesho unasikia majambazi wameuawa kwa risasi wakipambana na polisi,” alisema.
Matutu alihoji kuwa ikiwa Kenyalla kasema kweli kwenye taarifa yake, aeleze ni majambazi wangapi askari waliwakamata siku hiyo katika nyumba yake, kwa nini hawakuondoka na panga linalodaiwa lilitumika kuwajeruhi kama ushahidi? Polisi wanasaka watuhumiwa kwa kubomoa nyumba kwa mateke bila uongozi wa serikali ya eneo husika?
“Huyo Mama J waliyekuwa wakimtafuta hata siku ile alikuwepo lakini hawakumgusa licha ya kuwa tuhuma nyingi za kujihusidha na biashara haramu, leo Kamanda anadiriki kupotosha ukweli wa tukio na kuniita raia mwema jambazi?” alihoji.
Matutu alieleza kuwa hadi jana mchana walikuwa wamefika askari zaidi ya watatu wakidai wametumwa na wakubwa zao ili kumshawishi alifungue jalada la malalamiko kwa mdai kuwa uchunguzi unaendelea.
Matukio ya polisi kuua raia yamekuwa yakijirudia mara kwa mara nchini lakini licha ya wadau kutaka iundwe Tume Huru ya Uchunguzi wa Kimahakama ya mauaji hayo, serikali imekuwa ikikwepa na hivyo kuwapa polisi nafasi ya kujichunguza na kutoa ripoti.
Taarifa zote za vifo vya raia waliopigwa risasi na polisi hazijawahi kuwataja moja kwa moja wauaji badala yake wananchi huambiwa marehemu aligongwa na kitu kizito chenye ncha kali akapoteza uhai.
Alipotafutwa tena jana, Kenyela aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa sababu za kujeruhiwa kwa mwandishi huyo zilitokana na kumpiga askari kwa panga wakati wakiwa wanatekeleza wajibu wao.
Alisema taarifa walizopata kabla ya tukio hilo ni kwamba nyumba aliyokuwa akiishi Matutu kuna majambazi, hivyo mwandishi hakuwa na sababu ya kutoka na panga zaidi ya kujisalimisha na kujitambulisha kwa asakri hao.
Kenyela alisema kutokana na tukio hilo kwa sasa wapo katika uchunguzi na watakapobaini mkosaji ni nani katika kadhia hiyo watamchukulia hatua zinazostahili.
Kuhusu mtuhumiwa Mama J aliyekuwa amefananishwa na mke wa Matutu kutokana na kufanana kwa majina ya watoto wao, Kenyela alisema wanamfuatilia na watakapompata atawajibika juu ya mwenendo uliosababisha wananchi kumtilia shaka.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment