Friday, 28 December 2012

Mzungu anyongwa hoteli ya kitalii Dar

Raia  wa Bulgaria, Rola Cheterolia (42), mfanyakazi wa casino ya Kilimanjaro inayomilikiwa na Hoteli ya kitalii ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, amenyongwa na watu wasiojulikana.

Mwili wa mwanamke huyo ulikutwa katika nyumba za kupanga zilizoko eneo la hoteli hiyo ya kitalii iliyoko Masaki.

Habari zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa mwanamke huyo alinyongwa huku akiwa amefungwa mikono na miguu kwa kutumia kamba.

Marehemu alikuwa mfanyakazi wa casino hiyo na alikutwa na mkasa huo saa 3:00 usiku wa kuamkia jana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku.

“Tunasikitika sana kwa kitendo hiki kilichofanywa na watu hawa wasiojulikana cha huyu mwanamke wa kigeni kuuawa huko Sea Cliff, lakini bado tunafuatilia kwa kina kwani upelelezi unaendelea kubaini waliohusika katika tukio hilo,” alisema Kamanda Kenyela.

Kamanda Kenyela alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kwamba hakukuwa na dalili zozote za uvamizi ama ujambazi.

Hata hivyo, alisema kuna uwezekano wa tukio hilo kuwa la ulipizaji kisasi, lakini alisisitiza kuwa upepelezi bado unaendelea.

Alisema mlinzi wa eneo hilo alikimbia baada ya tukio hilo na Jeshi la Polisi linaendendelea kumsaka.

Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff ulipoulizwa jana kuhusiana na tukio hilo, ulithibitisha kutokea na kusema kwamba marehemu aliuawa juzi usiku.


Hata hivyo, uongozi wa hoteli hiyo haukutaka kueleza zaidi na kusema kwamba suala hilo wamelikabidhi kwenye vyombo vya usalama kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

“Ni kweli tukio hili limetokea pale `apartments' za Sea Cliff, na uchunguzi zaidi unaendelea, sisi hatuna cha kusema zaidi ya kukiri kwamba Rola ameuwa,” alisema mmoja wa watendaji waandamizi wa hoteli hiyo ambaye hata hivyo, hakutaka kutaja jina lake.

Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, mwili wa marehemu Rola umehifadhiwa katika Hospitali ya Hindu Mandal.

Wakati huo huo, Kamanda Kenyela alisema mtu mmoja ambaye hakufahamika jina lake, ameuawa na wananchi wenye hasira wakati akijaribu kuiba pikipiki.

Kamanda Kenyela alisema kuwa tukio hilo lilitokea eneo la Magomeni Makuti wilayani Kinondoni na kukemea kitendo hicho cha wananchi kujichukulia sheria mikononi.

Na katika hatua nyingine, Kamanda Kenyela alitoa ufafanuzi kuhusu tukio la kuibwa kwa mtoto mwenye umri wa siku 21.
Aliwataka wazazi kujifunza kupitia tukio hilo na wasimuamini mtu yeyote na kuwakabidhi watoto wao.

Alisema upelelezi unaendelea na kutoa rai kwa wananchi iwapo watamuona mtu yeyote akiwa na mtoto asiye wake, watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Tukio hilo lilitokea maeneo ya Mwenge baada ya mama wa mtoto huyo kumuomba mwanamke asiyefahamika amshikie mwanawe.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment