Tuesday 11 December 2012

Polisi wazidi kumwandama mwandishi


SIKU chache baada ya askari polisi wa mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kumjeruhi kwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Shaban Matutu, baadhi ya askari wanadaiwa kumfuatilia mwandishi huyo nyumbani kwake, jambo linalozua hofu ya usalama wa maisha yake.
Matutu alipigwa risasi na kujeruhiwa bega la kushoto wiki iliyopita wakati alipovamiwa na askari polisi wanne wenye silaha nyumbani kwake, wakidai kuwa walikuwa wanamsaka mtuhumiwa aitwaye Mama J anayedaiwa kuficha wahalifu nyumbani kwake.
Akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa kutolewa risasi hiyo mwilini, Matutu alidai kufuatwa na askari zaidi ya watatu kwa nyakati tofauti wakimweleza kuwa wametumwa na wakubwa zao wamshauri asichukue hatua yoyote ya kisheria.
Hata hivyo, wakati Matutu akidai kuwa askari hao wanaendelea kumfuatilia nyumbani kwake baada ya kutoka hospitali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Konondoni, Charles Kenyela, amesema hana habari ya kufuatwa kwa mwanahabari huyo.
Akizungumza na Tanzania Daima, Matutu alisema askari polisi hao walifika nyumbani kwake Ijumaa na Jumamosi wiki iliyopita na kumkuta mkewe na kuanza kumuuliza sehemu aliyoko mumewe.
Alisema kuwa baada ya kuuliza na kuambiwa hayupo, walitaka wapatiwe namba yake ya simu na kisha kuondoka lakini baadaye walirudi tena pasipo kueleza wanamtafuta kwa sababu gani.

“Walikuja mara mbili nyumbani kwangu wakajitambulisha mbele ya mke wangu na majirani kuwa wao ni askari na kwamba wananitafuta lakini hawakuacha maagizo niwakute katika kituo gani cha polisi,” alisema.
Matutu aliongeza kuwa kwa siku zote mbili walizofika nyumbani kwake, askari hao hawakutoa maelezo ni kituo gani wanachotoka au wanamhitaji kwa sababu gani.
Kufuatia hali hiyo ya kutia wasiwasi, Tanzania Daima lilimtafuta Kamanda Kenyela na kutaka kujua kama anafahamu harakati hizo za kutafutwa kwa Matutu.
Kenyela alisema hana taarifa za kutafutwa kwa Matutu na kwamba ikiwa atahitajika kwa ajili ya kutoa maelezo atataarifiwa kwa utaratibu.
“Kwa kweli sina la kuongea juu ya hilo mimi sina taarifa ya kutafutwa kwake na kama ana wasiwasi na watu hao ni vema afike katika kituo cha polisi na kutoa maelezo yatakayosaidia kuwabaini watu hao,” alisema.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment