Tuesday 11 December 2012

Wanafunzi kuwabaka walimu ni laana


Mbali na udhalilishaji huo, wanafunzi hao wamekuwa wakiwatishia maisha walimu hao, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto nyumba zao tatu. Habari zinasema walimu hao wamelazimika kuikimbia shule hiyo baada ya baadhi ya walimu wa kike kutongozwa na wanafunzi, kupigwa mabusu kwa nguvu hadharani, kutishiwa kuchomwa visu na kuchorwa vikatuni vya kudhalilisha.

Kutokana na hali hiyo, walimu wameshindwa kuvumilia udhalilishaji huo. Wamesema hali hiyo imeifanya shule hiyo kupoteza mwelekeo na kushindwa kutawalika, hivyo mazingira yake kuwa hatarishi, hasa kwa walimu wa kike.
Licha ya mamlaka husika kutotoa ushirikiano, walimu wamewalaumu wazazi wa wanafunzi hao kwa kusema wanawaunga mkono watoto wao. Na katika kuonyesha jinsi shule hiyo ilivyokubuhu kwa utovu wa nidhamu, miezi michache iliyopita wanafunzi walifanya mtihani wa kidato cha pili chini ya ulinzi wa askari polisi wenye silaha, kitu ambacho siyo cha kawaida katika hali yoyote ile.

Pamoja na ukweli kwamba tatizo la nidhamu haliko katika shule za kata pekee, tunadiriki kusema kwamba, kinyume na shule nyingine, shule hizo ndizo zenye tatizo kubwa la utovu wa nidhamu kutokana na mazingira hasi ambayo wanafunzi wa shule hizo wamejikuta. Kwa jumla, shule hizo zinaendesha mafunzo katika mazingira magumu mno kiasi cha watu wengi kuhoji kama kweli shule hizo zilianzishwa baada ya kufanyika matayarisho ya kutosha.

Hata hivyo, jambo moja lisilotia shaka ni kwamba Serikali ilikuwa na nia njema katika kuanzisha shule hizo za kata. Moja ya sababu ya hatua hiyo ya Serikali ilikuwa ni kuhakikisha kwamba maelfu kwa maelfu ya vijana wanaomaliza elimu ya msingi wapewe elimu ya sekondari ili hatimaye waweze kupata ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe katika mazingira ya kata zao, badala ya kukaa vijiweni.

Pamoja na nia njema hiyo, Serikali ilijikuta ikifanya kosa kubwa katika utekelezaji wa mradi huo wa Sekondari za Kata. Badala ya kutekeleza mradi huo kitaifa hatua kwa hatua, iliuchukulia mradi huo kama mtaji wake kisiasa na kama suala la kufa na kupona kwa kuamrisha mamlaka zote kuhakikisha kila mtu mzima anachanga fedha kwa ajili ya mradi huo.
Hata hivyo, wengi wanadhani kwamba kusuasua kwa mradi huo hadi hivi sasa kunatokana na ukweli kwamba ulianzishwa kwa malengo ya kisiasa zaidi na ndiyo maana wananchi wengi hawakuunga mkono. Kama tulivyodokeza hapo juu, shule hizo ziko katika hali mbaya kwa kukosa vitabu, walimu, madawati, madarasa, huduma za afya, chakula, miundombinu, usafiri na kadhalika. Hivyo, wanafunzi katika shule hizo wamejikuta njia panda wakizurura ovyo kwa kukosa walimu na kufanya vitendo vya kihalifu kama kutumia dawa za kulevya, wizi, ubakaji, uharibifu wa mali na uhasi dhidi ya mamlaka za shule hizo.

Sisi tunalaani vitendo hivyo kwa nguvu zote. Vitendo kama vilivyofanywa na wanafunzi wa Shule ya Ruaruke siyo tu ni laana kwa wanafunzi hao, bali pia havikubaliki. Wakati mamlaka husika zikichukua hatua dhidi ya wote waliohusika, ni matumaini yetu kwamba Serikali pia itahakikisha inaboresha mazingira ya sekondari zote za kata nchini ili ziwe na hadhi ya kuitwa shule. Vinginevyo, shule hizo zitaendelea kuwa vichaka vya wahuni na kukimbiwa na walimu wenye sifa.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment