Thursday 3 January 2013

Mama Pinda ataka wanaume wabadilike 2013


WANAUME nchini wametakiwa kuutumia mwaka 2013 kubadili mienendo na fikra zao juu ya wanawake, kwa kushirikiana nao katika shughuli za maendeleo badala ya kumuona mwanamke kuwa ni mtu asiyefaa katika harakati za maendeleo.
Wito huo ulitolewa jana na mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, katika Tamasha la Wanawake la Mwaka Mpya lililofanyika mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Alisema vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wanawake vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara, hali inayoonesha bado kundi hilo haliko salama kutokana na mfumo dume uliopo.
“Tumieni mwaka 2013 kwa kushauriana nyie kwa nyie kwa kila mwanamume kusema vipigo kwa wake zenu sasa basi, kwani huo si utu, mwanamke naye anapenda kuishi kwa amani kama mlivyo nyie wanaume na kama yupo mwanamke ambaye anamnyanyasa mumewe naye aache tabia hiyo,” alisema.
Alisema vitendo vya mwanamke kupigwa, kudhalilishwa kwa mambo yaliyo kinyume na haki za binadamu yamekuwa yakimsononesha mwanamke katika kuonesha uwezo wake alionao ambao angeweza kuutumia katika kujenga uchumi wa familia, jamii yake na taifa zima kwa ujumla.
Awali akimkaribisha Mama Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, alikiri kupokea msururu wa wanawake wanaohitaji msaada wa kisheria kutokana na kuporwa haki zao na wengine kunyanyaswa na wanaume kwa namna mbalimbali.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment