Wednesday, 27 February 2013

Waraka kwa JK, Sheikh Salum na Kard. Pengo

    
                                                 Alexander Joseph


NIANZE kwa kusema yeyote; Mkristo, Mwislamu au dini nyingine yoyote, wamekuwa katika dini zao baada ya kuwa wanadamu kwanza kabla ya kuwa waamini na wafuasi wa dini zao.
Dini bila utu, ni uhuni na ‘usanii’, hivyo, hakuna dini yoyote duniani inayoabudu kuua na kudhuru, kisha mhusika akajisifu kwa usahihi kuwa ana dini inayomtazama Mungu wa kweli.
Baada ya utangulizi huo, Rais Jakaya Kikwete nikwambie kwamba huenda husikii sauti za Watanzania wanaolia kutokana na tishio la kupotea amani nchini.
Si kwa kuwa husikii kwa sababu sauti hizo hazitoki, bali kwa vile hazikufikii sawasawa.
Watanzania wanakulilia wewe kwa kuwa tu, wewe ndiye mkuu wa nchi (baba mwenye nyumba) na mkubwa ni jaa, ndiyo maana tunakwambia wazi kuwa nchi inazidi kulowa kwa machozi huku harufu ya damu ikitishia kunuka.
Harufu ya damu inayotokana na vurugu, vita au mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ni mbaya na inatia kichechefu hasa inapomwagwa na ‘ndugu’ huku baadhi ya ndugu hao hao na majirani, wakijidai hawaoni wala kusikia lolote.
Wakabaki kuchungulia madirishani tu huku wengine wakidhani hawahusiki kumbe kupuuza jambo hili ni kujidanganya maana huu ni mtego wa panya, unawanasa waliomo na wasiokuwamo.
Kimsingi Rais wangu JK na viongozi wote wa dini, tulichokalia Watanzania si jiwe, bali bomu linalosubiri kulipuka. Tusaidieni, tuokoeni bomu hili lisilipuke, tutaangamia wote na Tanzania yetu tunayoipenda.
Hili ni bomu linalohitaji nia ya dhati na ushirikiano wa dhati baina ya serikali, viongozi wote wa dini za kweli na Watanzania wote wapenda amani ili kulitegua, vinginevyo litatulipukia wakati wowote.
Madhara yake, yana sifa ya kukosa ubaguzi, maana hayajali mtoto, mgonjwa, mzee, mlemavu, mjamzito, mwanamke, mwanamume, mwanasiasa wa upinzani au wa chama tawala wala dini ya mtu, iwe ya Kihindu, ya asili, Kiislamu au Kikristo. Wote wanaathirika. Hili, hatutaki litokee hapa Tanzania wala popote duniani.
Rais Kikwete, Ninajua wapo wanaokulaumu kwamba, “hujawatazama kwa jicho baya” wanaokuchafulia nchi kwa kuchochea, kuanzisha na kufanya vurugu, hasa za kidini, lakini binafsi naamini kwamba, unayoyasema, unayasema kwa dhati ingawa sijui ni kwanini wanaokuchafulia nchi na sifa wameamua kukuharibia.
Huenda wapo baadhi ya watu wanaotaka wewe na ‘kikundi chako cha kijani’ mharibikiwe kabisa ili wao waonekane ndio wazuri katika macho yetu.
Kwa utabiri wangu; huenda wengine ni ambao mnakunywa nao chai mchana, lakini usiku wanakuhujumu. Kabla hujaondoka kwenye ‘kiti ulichokalia’, wasake uwaumbue kwa tarumbeta za Unguja.
‘Baba mwenye nyumba’; Kikwete, kuwa mkali na fanya kwa vitendo kabisa moyoni, mdomoni, machoni na mikononi, watu hawa waache; najua wengine wanaweza kusema wakarudiarudia, bila lolote kubadilika lakini sauti yako ni sauti ya mamlaka ya umma, ukiitoa, nani atabisha?
Tunachohitaji na kuomba kwako, ni kusudio la dhati la kukomesha chokochoko hizo za kidini zinazokuchafulia nchi bila kujali mhusika ni wa chama cha upinzani, chama tawala, Mkristo, Mwislamu, Mkwere, Mkara, Mmakonde wala Mzanaki. Ukimchekea nyani utavuna mabua. Rais wangu, kumbuka wewe ni rais halali wa Watanzania wote na mamlaka halali.
Kwangu mimi, uadilifu na upendo wako kwa wa Tanzania wote si wa kutilia shaka hata kidogo na najua hakuna anayeweza kuwadanganya Watanzania wakubali kudanganywa kuwa na wewe unaugua ugonjwa wa udini ndiyo maana, macho ya Watanzania hasa Wakristo wanapolia, wanalia wakikutazama wewe lakini machozi yanailowanisha ardhi ya Tanzania unayoiongoza wewe.
Kwa waraka huu, nakuomba ukatae kabisa watu wasitumie dini kuigawa nchi yako katika vipande huku wakijadai wanampenda Mungu kumbe wanaigiza tu. Kwamba, ni wazi wanaofanya vurugu, ukatili na mauaji hayo yakiwamo ya viongozi wa dini, ni vibaraka wanaosaka ufadhili kutoka nje au ndani ya nchi ili nchi yako isitawalike; nao wapate cha kusema katika majukwaa ya kisiasa au kwa wafadhili wao.
Si siri, wanaofanya chokochoko hizi si tu kwamba wamekula sumu ya udini, bali pia wanamezeshwa sumu ya kisiasa na agenda yao ni pamoja na kuua Muungano, hivyo wanawaona baadhi ya Watanzania kama magugu katika malengo yao ya mavuno ya kisiasa na kiuchumi. Hii ni hatari na upotofu wa hali ya juu, ni kwa vile tu, hawajui walifanyalo.
Bahati nzuri watu hao ni wachache sana; hata huko visiwani Zanzibar, wanaoyafanya hayo ni wachache maana wengi ni watu wema na wanaochukizwa na unyama huo, lakini bahati mbaya ndani yake ni kwamba licha ya uchache wao, wana sumu kali ya ubaguzi na chokochoko za ubaguzi wa kidini zilizoficha siasa ndani yake na sumu hiyo inasambaa kwa kasi.
Rais wangu Kikwete; Rais usiyejikweza, usiyebagua wala kutaka makuu, usiruhusu yeyote abomoe nchi unayoijenga kwa mikono yako eti kwa kuwa tu, ni rafiki, ndugu, jirani, mtu wa kabila, chama chako au eti ni mtu wa dini yako. Usikubali kabisa.
Watumie wasaidizi wako wanuie kwa dhati kutafuta kwa kina chanzo cha tatizo hili kwa mapana na marefu yake vinginevyo, nchi inalowa chozi na kunuka damu ndani ya uongozi wako. Usikubali watangulizi wako wakucheke na kukusuta huku wakisema, “mbona kwetu haikutokea?”
Wasisitize Watanzania wanaojua na wasiojua kwamba, kuchezea amani hasa kwa misingi ya ubaguzi wa kidini, ni kufanya ujinga wa kujificha katika mdomo wa mamba mwenye njaa aliye mawindoni ukidhani uko salama kumbe umejizika mwenyewe kabla ya kufa.
Usikubali nchi itumbukie kwenye vita ya kidini ikiwa mikononi mwako. Hivi utamwambia nini Mungu! Hivi unajua kwamba hata wanaofanya mchezo huo bila hofu kana kwamba serikali imekwenda likizo wanajua kwamba wanaijeruhi Tanzania na Watanzania wake bila ubaguzi. Watanzania hatutaki vita ya udini, maana kwa asili, nchi yetu ni ya amani na upendo.
Unajua rais wangu tatizo ni kwamba, nchini kwetu tatizo la udini linazungumzwa kama hadithi katika siasa na vyombo vya habari ili kuombea kura, basi.
Ni wachache sana wenye nia ya dhati kuliondoa na ndiyo maana hata Jeshi la Polisi linapata kazi ngumu, licha ya juhudi zake zote kupambana na vurugu hizi.
Umefika wakati sasa serikali iache kufumba macho wala kuwavumilia wachochezi wote wa vurugu, ziwe za kidini au za kisiasa, hasa hao wanaotaka kuigawa Tanzania katika misingi ya dini.
Tanzania inalia machozi; inaaibika kimataifa. Itashindwa kujinasibu kama watu wake ni wacha Mungu. Wacha Mungu gani wanaokuwa tayari kupiga au kuua wenzao kwa kutumia jina la dini!
Watanzania tutachekwa na wakati huo tukiwa tunaficha nyuso zetu kwa viganja vya mikono.
Wapo waamini wengi wa Kiislamu (waamini wa kweli) wanaoishi kwa hofu kutoka kwa wenzao wanaojaribu kufanya chokochoko na vurugu za kidini kwa vile tu, hawataki kuunga mkono uchafu huo ndani ya nchi na mbele ya Mungu.
chanzo:daima 

No comments:

Post a Comment