Monday, 11 March 2013

Askofu Mkuu wa Anglikana avamiwa na majambazi


Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa, amevamiwa na majambazi nyumbani kwake, Mbezi kwa Yusufu, Kimara jijini Dar es Salaam usiku wa uamkia jana.
Katika tukio hilo, mlinzi wa askofu, amejeruhiwa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni katika kumshinikiza aonyeshe alipo Askofu Mokiwa.
Kwa mujibu wa Askofu Mokiwa, tukio hilo lilitokea jana saa 8:45 usiku ambapo watu hao walikata uzio na kufanikiwa kuingia kwenye uwanja wa nyumba yake.
Alisema baada ya watu hao ambao idadi yake haifahamu kuingia ndani ya uzio, walikutana na mlinzi na kumshinikiza awaonyeshe alipo yeye (askofu). Aliongeza kuwa, mlinzi huyo baada ya kuwaeleza watu hao kuwa, askofu hayupo, walianza kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
“Wamemjeruhi mshipa wa mguu wa kushoto, sehemu za kichwani na kukata kidole, wakati haya yakiendelea mlinzi wangu alipiga kelele ambazo ziliwezesha kumshtua mke wangu na mlinzi mwingine wa jirani yangu,” alisema.
Mokiwa alisema baada ya mke wake kusikia kelele hizo, alimuamsha na baada ya watu hao kubaini hilo, walikimbia kusikojulikana. Alisema walitoa taarifa kituo cha polisi Mbezi Luis ambapo polisi walitoa ushirikiano.
“Baada ya polisi kutupa PF3 tulimpeleka majeruhi hospitali ya Tumbi, Kibaha ambapo hapo alitibiwa na kuruhusiwa, hali yake sio mbaya ingawa analalamika anamaumivu makali maeneo yenye majeraha,” alisema.
Askofu Mokiwa akizungumzia kuhusiana na kauli za watuhumiwa hao kumtaka yeye baada ya kuingia kwenye nyumba yake, alisema anafiriki watu hao watakuwa wametumwa na mtu.
“Nadhani wametumwa lakini sijui ni nani amefanya hivyo, kiukweli sina chuki, uadui wala kinyongo na mtu yeyote, ninaishi na watu wangu vizuri, sijui haya yanayotokea yanalenga nini,” alisema.
Alisema katika maisha yake tukio la kuvamiwa ni la kwanza na kwake amesema ni la aina yake.
Aidha, wakati akizungumza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu majira ya saa 8: 15 mchana, Askofu Mokiwa alisema polisi wamewasili nyumbani hapo kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, analifuatilia.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment