ASKARI wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), wamewasili Zanzibar kufanya uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki.
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kwa simu jana kuwa wapelelezi wa kigeni wamewasili Zanzibar na tayari na wameanza kazi hiyo.
Wapelelezi hao wameingia kazini kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri huyo aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.
Padri Mushi aliuawa asubuhi alipokuwa akienda kuongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Teresia, Beit el Raas, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuzikwa Kitope, Kaskazini Unguja Februari 20, mwaka huu.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” Kamishna Mussa alisema bila ya kutaja wanatoka nchi gani.
Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni lini wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni siri za Polisi na zikivuja, zitaingilia uchunguzi wanaoufanya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya Serikali, vililithibitishia gazeti hili kuwa FBI walikuwa wameanza kuwasaka wauaji wa Padri Mushi.
Kutua kwa wapelelezi hao wa Marekani kunafuatia kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.
Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alihusisha tukio hilo na vitendo vya ugaidi wakati akitoa tamko la Serikali na kueleza kuwa Rais Kikwete ameidhinisha Serikali kugharamia wapelelezi kutoka nje.
Pia ujio wa FBI unaweza kuhusishwa moja kwa moja na dhamira iliyoonyeshwa mapema na Serikali ya Marekani iliyokuwa tayari kusaidia upelelezi wa mauaji hayo na hiyo ilibainishwa katika salamu za rambirambi za kifo hicho na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Serikali vimeeleza kuwa kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, maofisa wa FBI walifanya mazungumzo na Waziri Nchimbi na viongozi wengine wa Serikali kwa ajili ya kuangalia ni namna gani watafanya shughuli hiyo.
“Pia hawa jamaa wa FBI walifanya vikao na maofisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ili kuweka sawa mazingira ya kufanya upelelezi huu,” kilisema chanzo kingine.
Habari zaidi zinaeleza kuwa uchunguzi wa wapelelezi hao wa FBI na wale wa Tanzania hautajikita katika kusaka wauaji wa Padri Mushi pekee, bali watakwenda mbali zaidi na kuchunguza wale wote wanaojihusisha na wimbi la vurugu za kidini nchini ambalo linatishia amani.
Hii itakuwa mara ya pili kwa FBI kuja nchini kufanya operesheni kubwa ya upelelezi. Mwaka 1998 walifika kuchunguza kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani na kugundua kuwa Kundi la Al-Qaeda lilihusika.
Aidha hiyo ni mara ya tatu kwa wapelelezi wa Tanzania kushirikiana na wageni kuchunguza matukio ya uhalifu baada ya mwaka 1984, Idara ya Upelelezi ya Uingereza, Scotland Yard ya Uingereza kuchunguza kuungua kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Habari zaidi zinaeleza kuwa kabla ya ujio wa FBI, Serikali ya Tanzania ilizungumza na taasisi za upelelezi za nchi tano ili kuongeza nguvu. Taasisi nyingine zinazodaiwa kuombwa kufanya kazi hiyo ni pamoja na Scotland Yard na Shirika la Upelelezi la Israel, Mossad.
Akizungumzia upelelezi wa mauaji ya Padri Mushi, Kamishna Mussa alisema watu kadhaa wametiwa mbaroni kwa mauaji lakini asingeweza kutaja idadi.
Kuuawa kwa padri huyo ni miongoni mwa matukio ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini huko Zanzibar baada ya kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti, Fadhil Soraga, kupigwa risasi kwa Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki na kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis shambani kwake huko Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment